Mit 23:1-18
Mit 23:1-18 SUV
Utakapoketi kwa chakula pamoja na mtawala, Mwangalie sana yeye aliye mbele yako. Tena ujitie kisu kooni, Kama ukiwa mlafi. Usivitamani vyakula vyake vya anasa; Kwa maana ni vyakula vya hila. Usijitaabishe ili kupata utajiri; Acha kuzitegemea akili zako mwenyewe. Je! Utavikazia macho vile ambavyo si kitu? Maana bila shaka mali hujifanyia mabawa, Kama tai arukaye mbinguni. Usile mkate wa mtu mwenye husuda; Wala usivitamani vyakula vyake vya anasa; Maana aonavyo nafsini mwake, ndivyo alivyo. Akuambia, Haya, kula, kunywa; Lakini moyo wake hauwi pamoja nawe. Tonge lile ulilokula utalitapika, Na maneno yako matamu yatakupotea. Usiseme masikioni mwa mpumbavu; Maana atadharau hekima ya maneno yako. Usiiondoe alama ya mpaka wa zamani; Wala usiingie katika mashamba ya yatima; Kwa sababu mkombozi wao ana nguvu; Atawatetea juu yako. Elekeza moyo wako kusikiliza mafundisho; Tega masikio yako kusikia maneno ya maarifa. Usimnyime mtoto wako mapigo; Maana ukimpiga kwa fimbo hatakufa. Utampiga kwa fimbo, Na kumwokoa nafsi yake na Kuzimu. Mwanangu, kama moyo wako una hekima, Moyo wangu utafurahi, naam, moyo wangu; Naam, viuno vyangu vitafurahi, Midomo yako inenapo maneno mema. Moyo wako usiwahusudu wenye dhambi; Bali mche BWANA mchana kutwa; Maana bila shaka iko thawabu; Na tumaini lako halitabatilika.