Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Hes 10:11-36

Hes 10:11-36 SUV

Ikawa mwaka wa pili, mwezi wa pili, siku ya ishirini ya mwezi, hilo wingu liliinuka kutoka pale juu ya maskani ya ushahidi. Wana wa Israeli wakasafiri kwenda mbele, kwa safari zao kutoka jangwa la Sinai; na hilo wingu likakaa katika jangwa la Parani. Nao wakasafiri kwanza kwa amri ya BWANA kwa mkono wa Musa. Mahali pa mbele ilisafiri beramu ya marago ya wana wa Yuda, kwa majeshi yao; na Nashoni mwana wa Aminadabu ndiye aliyekuwa juu ya jeshi lake. Na juu ya jeshi la kabila ya wana wa Isakari alikuwa Nethaneli mwana wa Suari. Na juu ya jeshi la kabila ya wana wa Zabuloni ni Eliabu mwana wa Heloni. Na maskani ilishushwa; na wana wa Gershoni, na wana wa Merari, walioichukua maskani, wakasafiri kwenda mbele. Kisha beramu ya marago ya Reubeni ikasafiri kwenda mbele kwa majeshi yao; na juu ya jeshi lake alikuwa Elisuri mwana wa Shedeuri. Tena juu ya jeshi la kabila ya wana wa Simeoni ni Shelumieli mwana wa Suri-shadai. Tena juu ya jeshi la kabila ya wana wa Gadi ni Eliasafu mwana wa Deueli. Ndipo wakasafiri Wakohathi wenye kuvichukua vile vitu vitakatifu; na hao wengine wakaisimamisha maskani kabla hawajaja wao. Kisha beramu ya marago ya wana wa Efraimu ikasafiri kwenda mbele kwa majeshi yao; na juu ya jeshi lake ni Elishama mwana wa Amihudi. Tena juu ya jeshi la kabila ya wana wa Manase ni Gamalieli mwana wa Pedasuri. Tena juu ya jeshi la kabila ya wana wa Benyamini ni Abidani mwana wa Gideoni. Kisha beramu ya marago ya wana wa Dani, ambayo yalikuwa ni nyuma ya marago yote, ikasafiri, kwa majeshi yao; na juu ya jeshi lake ni Ahiezeri mwana wa Amishadai. Tena juu ya jeshi la kabila ya wana wa Asheri ni Pagieli mwana wa Okrani; Tena juu ya jeshi la kabila ya wana wa Naftali ni Ahira mwana wa Enani. Ndivyo zilivyokuwa safari zao wana wa Israeli kwa majeshi: yao; nao wakasafiri kwenda mbele. Kisha Musa akamwambia Hobabu, mwana wa Reueli Mmidiani, mkwewe Musa, Sisi twasafiri kwenenda mahali ambapo BWANA amenena habari zake hivi, Nitawapa ninyi mahali hapo; uje pamoja nasi, nasi tutakufanyia mema; kwa kuwa BWANA ametamka mema juu ya Israeli. Naye akamwambia, Siendi mimi; ila nitairudia nchi yangu mwenyewe, na kwa jamaa zangu mwenyewe. Naye akamwambia, Usituache, tafadhali; kwa kuwa wewe wajua jinsi tutakavyopanga nyikani, nawe utakuwa kwetu badala ya macho. Itakuwa, ukienda pamoja nasi, naam, itakuwa mema yo yote BWANA atakayotutendea sisi, tutakutendea wewe vivyo. Basi wakasafiri kutoka penye mlima wa BWANA safari ya siku tatu; na sanduku la agano la BWANA likatangulia mbele yao mwendo wa siku tatu, ili kuwatafutia mahali pa kupumzika. Na wingu la BWANA lilikuwa juu yao mchana hapo waliposafiri kwenda mbele kutoka kambini. Ilikuwa, hapo sanduku liliposafiri kwenda mbele, ndipo Musa akasema, Inuka, Ee BWANA, adui zako na watawanyike; na wakimbie mbele zako hao wakuchukiao. Tena hapo liliposimama, akasema, Ee BWANA, uwarudie maelfu kumi ya maelfu ya Israeli.

Soma Hes 10

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha