Neh 8:4-8
Neh 8:4-8 SUV
Naye Ezra, kuhani, akasimama juu ya mimbari ya mti, waliyokuwa wameifanya kwa kusudi hilo; na karibu naye wakasimama Matithia, na Shema, na Anaya, na Uria, na Hilkia, na Maaseya, mkono wake wa kuume; na mkono wake wa kushoto, Pedaya, na Misbaeli, na Malkiya, na Hashumu, na Hashbadani, na Zekaria, na Meshulamu. Ezra akakifunua kitabu machoni pa watu wote; (maana alikuwa juu ya watu wote); na hapo alipokifungua, watu wote walisimama; Ezra akamhimidi BWANA, Mungu Mkuu. Nao watu wote wakaitika, Amina, Amina, pamoja na kuinua mikono yao; kisha wakainama vichwa vyao, wakamsujudu BWANA kifudifudi. Tena Yeshua, na Bani, na Sherebia, na Yamini, na Akubu, na Shabethai, na Hodai, na Maaseya, na Kelita, na Azaria, na Yozabadi, na Hanani, na Pelaya, nao ni Walawi, wakawafahamisha watu torati; na watu wakasimama mahali pao. Nao wakasoma katika kitabu, katika torati ya Mungu, kwa sauti ya kusikilika; wakaeleza maana yake, hata wakayafahamu yaliyosomwa.