Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mk 1:1-20

Mk 1:1-20 SUV

Mwanzo wa Injili ya Yesu Kristo, Mwana wa Mungu. Kama ilivyoandikwa katika nabii Isaya, Tazama, namtuma mjumbe wangu Mbele ya uso wako, Atakayeitengeneza njia yako. Sauti ya mtu aliaye nyikani, Itengenezeni njia ya Bwana, Yanyosheni mapito yake. Yohana alitokea, akibatiza nyikani, na kuuhubiri ubatizo wa toba liletalo ondoleo la dhambi. Wakamwendea nchi yote ya Uyahudi, nao wa Yerusalemu wote, wakabatizwa katika mto wa Yordani, wakiziungama dhambi zao. Na Yohana alikuwa amevaa singa za ngamia na mshipi wa ngozi kiunoni mwake, akala nzige na asali ya mwitu. Akahubiri akisema, Yuaja nyuma yangu aliye na nguvu kuliko mimi, ambaye mimi sistahili kuinama na kuilegeza gidamu ya viatu vyake. Mimi niliwabatiza kwa maji; bali yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu. Ikawa siku zile, Yesu alikuja kutoka Nazareti ya Galilaya, akabatizwa na Yohana katika Yordani. Mara alipopanda kutoka majini, akaona mbingu zinapasuka, na Roho, kama hua, akishuka juu yake; na sauti ikatoka mbinguni, Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe. Mara Roho akamtoa aende nyikani. Akawako huko jangwani siku arobaini, hali akijaribiwa na Shetani; naye alikuwa pamoja na wanyama wa mwitu, na malaika walikuwa wakimhudumia. Hata baada ya Yohana kutiwa gerezani, Yesu akaenda Galilaya, akiihubiri Habari Njema ya Mungu, akisema, Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni, na kuiamini Injili. Naye alipokuwa akipita kando ya bahari ya Galilaya, akamwona Simoni na Andrea nduguye, wakitupa jarife baharini; kwa maana walikuwa wavuvi. Yesu akawaambia, Njoni mnifuate, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu. Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata. Akaendelea mbele kidogo, akamwona Yakobo wa Zebedayo, na Yohana nduguye, nao pia walikuwa chomboni, wakizitengeneza nyavu zao. Mara akawaita, wakamwacha baba yao Zebedayo ndani ya chombo pamoja na watu wa mshahara, wakaenda, wakamfuata.

Soma Mk 1

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Mk 1:1-20

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha