Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Lk 7:1-30

Lk 7:1-30 SUV

Alipokwisha kuyamaliza maneno yake yote masikioni mwa watu, aliingia Kapernaumu. Na mtumwa wake akida mmoja alikuwa hawezi, karibu na kufa; naye ni mtu aliyempenda sana. Aliposikia habari za Yesu, alituma wazee wa Wayahudi kwake kumwomba aje amponye mtumwa wake. Nao walipofika kwa Yesu, walimsihi sana wakisema, Amestahili huyu umtendee neno hili; maana, analipenda taifa letu, naye alitujengea sinagogi. Basi Yesu akaenda pamoja nao. Hata alipokuwa si mbali na nyumba yake, yule akida alituma rafiki kwake, akamwambia, Bwana, usijisumbue, maana mimi sistahili wewe uingie chini ya dari yangu; kwa hiyo nilijiona sistahili mwenyewe kuja kwako; lakini, sema neno tu, na mtumwa wangu atapona. Kwa maana mimi nami ni mtu niliyewekwa chini ya mamlaka, mwenye askari chini yangu; nikimwambia huyu, Nenda, huenda; na huyu, Njoo, huja; na mtumwa wangu, Fanya hivi, hufanya. Yesu aliposikia hayo alimstaajabia, akaugeukia mkutano uliokuwa ukimfuata, akasema, Nawaambia, hata katika Israeli sijaona imani kubwa namna hii. Na wale waliotumwa waliporudi nyumbani, wakamkuta yule mtumwa ni mzima. Baadaye kidogo alikwenda mpaka mji mmoja uitwao Naini, na wanafunzi wake walifuatana naye pamoja na mkutano mkubwa. Na alipolikaribia lango la mji, hapo palikuwa na maiti anachukuliwa nje, ni mwana pekee wa mamaye ambaye ni mjane, na watu wa mjini wengi walikuwa pamoja naye. Bwana alipomwona alimwonea huruma, akamwambia, Usilie. Akakaribia, akaligusa jeneza; wale waliokuwa wakilichukua wakasimama. Akasema, Kijana, nakuambia, Inuka. Yule maiti akainuka, akaketi, akaanza kusema. Akampa mama yake. Hofu ikawashika wote, wakamtukuza Mungu, wakisema, Nabii mkuu ametokea kwetu; na, Mungu amewaangalia watu wake. Habari hii yake ikaenea katika Uyahudi wote, na katika nchi zote za kando kando. Wanafunzi wa Yohana wakamletea habari za hayo yote. Ndipo Yohana alipowaita wawili katika wanafunzi wake, akawatuma kwa Yesu akiuliza, Wewe ndiwe yule ajaye, au tumtazamie mwingine? Nao walipofika kwake, walisema, Yohana Mbatizaji ametutuma kwako, akisema, Wewe ndiwe yule ajaye, au tumtazamie mwingine? Na saa ile ile aliwaponya wengi magonjwa yao, na misiba, na pepo wabaya; na vipofu wengi aliwakirimia kuona. Ndipo alipojibu, akawaambia, Nendeni mkamweleze Yohana hayo mliyoyaona na kuyasikia; vipofu wanapata kuona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakasika, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa, maskini wanahubiriwa habari njema. Naye heri mtu ye yote asiyechukizwa nami. Basi, wajumbe wa Yohana walipokwisha ondoka, alianza kuwaambia makutano habari za Yohana, Mlitoka kwenda nyikani kutazama nini? Unyasi ukitikiswa na upepo? Lakini mlitoka kwenda kuona nini? Mtu aliyevikwa mavazi mororo? Jueni, watu wenye mavazi ya utukufu, wanaokula raha, wamo katika majumba ya kifalme. Lakini, mlitoka kwenda kuona nini? Nabii? Naam, nawaambia, na aliye zaidi ya nabii. Huyo ndiye aliyeandikiwa haya, Tazama, namtuma mjumbe wangu Mbele ya uso wako, Atakayeitengeneza njia yako mbele yako. Nami nawaambia, Katika wale waliozaliwa na wanawake hakuna aliye mkuu kuliko Yohana; lakini aliye mdogo katika ufalme wa Mungu ni mkuu kuliko yeye. Na watu wote na watoza ushuru waliposikia hayo, waliikiri haki ya Mungu, kwa kuwa wamebatizwa kwa ubatizo wa Yohana. Lakini, Mafarisayo na wana-sheria walilipinga shauri la Mungu juu yao, kwa kuwa hawakubatizwa naye.

Soma Lk 7