Ayu 31:24-40
Ayu 31:24-40 SUV
Ikiwa nimeifanya dhahabu kuwa tumaini langu, Na kuiambia dhahabu safi, Wewe u tegemeo langu; Kama nilifurahi kwa kuwa mali yangu yalikuwa mengi, Na kwa sababu mkono wangu umepata vitu vingi; Kama nililitazama jua lilipoangaza, Au mwezi ukiendelea katika kung’aa; Na moyo wangu umeshawishwa kwa siri, Na midomo yangu imeubusu mkono wangu; Hilo nalo lingekuwa uovu wa kuadhibiwa na waamuzi; Kwani ningemwambia uongo Mungu aliye juu. Kama nilifurahi kwa kuangamia kwake huyo aliyenichukia, Au kujitukuza alipopatikana na maovu; (Naam, sikukiacha kinywa changu kufanya dhambi Kwa kuutaka uhai wake kwa kuapiza); Kama watu wa hemani mwangu hawakunena, Ni nani awezaye kumpata mtu asiyeshibishwa na yeye kwa nyama? Mgeni hakulala njiani; Lakini nilimfungulia msafiri milango yangu; Ikiwa kama mwanadamu nimeyafunika makosa yangu, Kwa kuuficha uovu wangu kifuani mwangu; Kwa sababu niliwaogopa mkutano mkubwa, Na dharau la jamaa lilinitia hofu, Hata nilinyamaa kimya, nisitoke mlangoni- Laiti ningekuwa na mtu wa kunisikia! (Tazama, sahihi yangu ni hii, Mwenyezi na anijibu); Laiti ningekuwa na hayo mashitaka yaliyoandikwa na adui yangu! Hakika ningeyachukua mabegani; Ningejifungia mfano wa kilemba. Ningemwambia hesabu ya hatua zangu Ningemkaribia kama vile mkuu. Kama nchi yangu yalia juu yangu, Na matuta yake hulia pamoja; Kama nimeyala matunda yake pasipo kulipa, Au kama nimewafanya wenyewe kupotewa na uhai; Miiba na imee badala ya ngano, Na magugu badala ya shayiri. Maneno ya Ayubu yamekoma hapa.