Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yn 11:1-27

Yn 11:1-27 SUV

Basi mtu mmoja alikuwa hawezi, Lazaro wa Bethania, mwenyeji wa mji wa Mariamu na Martha, dada yake. Ndiye Mariamu yule aliyempaka Bwana marhamu, akamfuta miguu kwa nywele zake, ambaye Lazaro nduguye alikuwa hawezi. Basi wale maumbu wakatuma ujumbe kwake wakisema, Bwana, yeye umpendaye hawezi. Naye Yesu aliposikia, alisema, Ugonjwa huu si wa mauti, bali ni kwa ajili ya utukufu wa Mungu, ili Mwana wa Mungu atukuzwe kwa huo. Naye Yesu alimpenda Martha na umbu lake na Lazaro. Basi aliposikia ya kwamba hawezi, alikaa bado siku mbili pale pale alipokuwapo. Kisha, baada ya hayo, akawaambia wanafunzi wake, Twendeni Uyahudi tena. Wale wanafunzi wakamwambia, Rabi, juzijuzi tu Wayahudi walikuwa wakitafuta kukupiga kwa mawe, nawe unakwenda huko tena? Yesu akajibu, Je! Saa za mchana si kumi na mbili? Mtu akienda mchana hajikwai; kwa sababu aiona nuru ya ulimwengu huu. Bali akienda usiku hujikwaa; kwa sababu nuru haimo ndani yake. Aliyasema hayo; kisha, baada ya hayo, akawaambia, Rafiki yetu, Lazaro, amelala; lakini ninakwenda nipate kumwamsha. Basi wale wanafunzi wakamwambia, Bwana, ikiwa amelala, atapona. Lakini Yesu alikuwa amenena habari ya mauti yake; nao walidhania ya kuwa ananena habari ya kulala usingizi. Basi hapo Yesu akawaambia waziwazi, Lazaro amekufa. Nami nafurahi kwa ajili yenu kwamba sikuwako huko, ili mpate kuamini; lakini na twendeni kwake. Basi Tomaso, aitwaye Pacha, akawaambia wanafunzi wenziwe, Twendeni na sisi, ili tufe pamoja naye. Basi Yesu alipofika, alimkuta amekwisha kuwamo kaburini yapata siku nne. Na Bethania ilikuwa karibu na Yerusalemu, kadiri ya maili mbili hivi; na watu wengi katika Wayahudi walikuwa wamekuja kwa Martha na Mariamu, ili kuwafariji kwa habari ya ndugu yao. Basi Martha aliposikia kwamba Yesu anakuja, alikwenda kumlaki; na Mariamu alikuwa akikaa nyumbani. Basi Martha akamwambia Yesu, Bwana, kama ungalikuwapo hapa, ndugu yangu hangalikufa. Lakini hata sasa najua ya kuwa yo yote utakayomwomba Mungu, Mungu atakupa. Yesu akamwambia, Ndugu yako atafufuka. Martha akamwambia, Najua ya kuwa atafufuka katika ufufuo siku ya mwisho. Yesu akamwambia, Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi; naye kila aishiye na kuniamini hatakufa kabisa hata milele. Je! Unayasadiki hayo? Akamwambia, Naam, Bwana, mimi nimesadiki ya kwamba wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu, yule ajaye ulimwenguni.

Soma Yn 11

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Yn 11:1-27

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha