Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Amu 9:22-57

Amu 9:22-57 SUV

Basi Abimeleki alitawala juu ya Israeli muda wa miaka mitatu. Kisha Mungu akapeleka roho mbaya kati ya Abimeleki na watu wa Shekemu; nao watu wa Shekemu wakamtendea Abimeleki kwa udanganyifu; ili kwamba huo udhalimu waliotendewa hao wana sabini wa Yerubaali uje, tena kwamba damu yao iandikwe juu ya Abimeleki ndugu yao, aliyewaua, na juu ya watu wa Shekemu, waliomtia nguvu mikono yake ili awaue hao nduguze. Basi watu wa Shekemu wakaweka watu kumvizia juu ya vilele vya milima, ambao waliwanyang’anya vitu vyao watu wote waliopita njia hiyo karibu nao; naye Abimeleki aliambiwa. Kisha Gaali, mwana wa Ebedi, akaenda pamoja na nduguze, wakavuka na kufika Shekemu; na watu wa Shekemu wakamtumaini yeye. Nao wakatoka kwenda mashambani, wakavuna mashamba yao ya mizabibu, na kuzishindika hizo zabibu, na kufanya sikukuu, kisha wakaingia nyumbani mwa mungu wao, wakala na kunywa na kumlaani huyo Abimeleki. Naye Gaali mwana wa Ebedi akasema, Abimeleki ni nani, na Shekemu ni nani, hata tukamtumikie yeye? Yeye, je! Si mwana wa Yerubaali? Na Zebuli siye akida wake? Haya, ninyi watumikieni hao watu wa Hamori, babaye Shekemu; Lakini sisi je! Tumtumikie kwa sababu gani? Laiti watu hawa wangekuwa chini ya mkono wangu! Hapo basi mimi ningemwondoa huyo Abimeleki. Kisha akamwambia Abimeleki, Haya, ongeza askari zako, utoke nje. Basi hapo Zebuli, aliyekuwa liwali wa mji, alipoyasikia hayo maneno ya Gaali mwana wa Ebedi, hasira zake zikamwaka. Naye akatuma wajumbe waende kwa Abimeleki kwa siri, akasema, Tazama, Gaali, mwana wa Ebedi, na ndugu zake wamekuja Shekemu; na tazama waufitinisha mji huu kinyume chako. Basi sasa, inuka wewe, usiku, wewe na watu walio pamoja nawe, mvizie mashambani; kisha itakuwa, asubuhi, mara litakapokucha jua, wewe utaamka asubuhi na mapema, na kuushambulia mji huo; tena, angalia, hapo yeye na wale watu walio pamoja naye watakapokutokea nje kupigana nawe, ndipo utapata kuwatenda kama utakavyopata nafasi. Basi Abimeleki akainuka na watu wote waliokuwa pamoja naye, usiku nao wakauvizia Shekemu kwa vikosi vinne. Huyo Gaali mwana wa Ebedi akatoka nje, akasimama penye maingilio ya lango la mji; naye Abimeleki na hao watu waliokuwa pamoja naye wakainuka kutoka mahali pale walipokuwa wanavizia. Basi Gaali alipowaona hao watu, akamwambia Zebuli, Tazama, watu washuka kutoka katika vilele vya milima. Zebuli akamwambia, Ni kivuli cha milima unachokiona kama ndio watu. Kisha Gaali akasema mara ya pili, akanena, Angalia, watu washuka katikati ya nchi, na kikosi kimoja kinakuja kwa njia ya mwaloni wa Meonenimu. Ndipo Zebuli akamwambia, Je! Kinywa chako sasa ki wapi, hata ukasema Huyo Abimeleki ni nani, hata inatupasa kumtumikia yeye? Je! Hawa sio watu hao uliowadharau wewe? Haya, toka nje sasa, tafadhali, upigane nao. Basi Gaali akatoka nje mbele ya watu wa Shekemu, akapigana na Abimeleki. Lakini Abimeleki akamkimbiza, naye akakimbia mbele yake, wengi wakaanguka waliojeruhiwa hata kufikilia maingilio ya hilo lango. Abimeleki akakaa Aruma; naye Zebuli akawatoa Gaali na ndugu zake, wasikae katika Shekemu. Ikawa siku ya pili yake, watu wakatoka waende mashambani; naye Abimeleki aliambiwa. Naye akawatwaa watu wake, na kuwagawanya wawe vikosi vitatu, nao wakavizia mashambani; naye akaangalia, na tazama, watu walikuwa watoka humo mjini; basi akainuka na kupigana nao, akawapiga. Abimeleki, na vile vikosi vilivyokuwa pamoja naye, wakafuliza kwenda mbele, wakasimama penye maingilio ya lango la mji, na vile vikosi viwili vikawarukia hao wote waliokuwa mashambani, na kuwapiga. Abimeleki akapigana na huo mji mchana kutwa; akautwaa mji, akawaua watu waliokuwamo ndani yake; kisha akaupomosha mji, na kuutia chumvi. Kisha watu wote waliokaa katika ile buruji ya Shekemu waliposikia habari hiyo wakaingia ndani ya ngome ya nyumba ya El-berithi. Abimeleki aliambiwa ya kuwa watu hao wote wa buruji ya Shekemu wamekutana pamoja. Basi Abimeleki akakwea kwenda kilima cha Salmoni, yeye na wote waliokuwa pamoja naye; naye Abimeleki akashika shoka mkononi mwake, akakata tawi moja katika miti, akalishika na kujitweka fuzini mwake; akawaambia hao watu waliokuwa pamoja naye, Haya, mliyoniona mimi kufanya, fanyeni upesi vivyo, kama nilivyofanya mimi. Basi watu hao wote vivyo wakakata kila mtu tawi lake, wakamwandama Abimeleki, wakayaweka hayo matawi pale ngomeni, na kuiteketeza moto hiyo ngome juu yao; basi hivyo watu wote wa hiyo buruji ya Shekemu wakafa, walipata kama watu elfu, waume kwa wake. Ndipo Abimeleki alipokwenda Thebesi, akapanga kinyume cha Thebesi na kuutwaa. Lakini ndani ya huo mji palikuwa na buruji yenye nguvu, na watu wote waume na wake wakakimbilia huko, na watu wote wa mji, nao wakajifungia ndani, wakapanda paa la buruji. Abimeleki akaiendea hiyo buruji na kupigana nayo; naye akaukaribia mlango wa buruji ili auteketeze kwa moto. Na mwanamke mmoja akabwaga jiwe la kusagia la juu, nalo likampiga Abimeleki kichwani, na kulivunja fuvu la kichwa chake. Ndipo akamwita kwa haraka huyo kijana aliyekuwa anamchukulia silaha zake, na kumwambia, Futa upanga wako, uniue, ili watu wasiseme juu yangu Aliuawa na mwanamke. Basi huyo kijana wake akamchoma upanga, naye akafa. Basi hapo watu wa Israeli walipoona ya kuwa Abimeleki amekufa, wakaondoka wakaenda kila mtu mahali pake. Basi hivyo Mungu akalipiza kisasi juu ya uovu wa Abimeleki aliomtenda baba yake, katika kuwaua hao nduguze watu sabini; uovu wote wa watu wa Shekemu Mungu alilipiza juu ya vichwa vyao; na hiyo laana ya Yothamu mwana wa Yerubaali ikawajilia juu yao.

Soma Amu 9

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha