Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Amu 2:10-23

Amu 2:10-23 SUV

Tena watu wote wa kizazi hicho nao walikusanywa waende kwa baba zao; kikainuka kizazi kingine nyuma yao, ambacho hakikumjua BWANA, wala hawakuijua hiyo kazi ambayo alikuwa ameitenda kwa ajili ya Israeli. Wana wa Israeli walifanya yaliyokuwa ni maovu mbele za macho ya BWANA, nao wakawatumikia Mabaali. Wakamwacha BWANA, Mungu wa baba zao, aliyewaleta kutoka katika nchi ya Misri, wakafuata miungu mingine, baadhi ya miungu ya watu wale waliokaa karibu nao pande zote, wakajiinamisha mbele yao; wakamkasirisha BWANA, akaghadhibika. Wakamwacha BWANA, wakamtumikia Baali na Maashtorethi. Hasira ya BWANA ikawaka juu ya Israeli, naye akawatia katika mikono ya watu waliowateka nyara, akawauza na kuwatia katika mikono ya adui zao pande zote; hata wasiweze tena kusimama mbele ya adui zao. Kila walikokwenda mkono wa BWANA ulikuwa juu yao kuwatenda mabaya, kama BWANA alivyosema, na kama BWANA alivyowaapia; nao wakafadhaika sana. Kisha BWANA akawainua waamuzi, waliowaokoa na mikono ya watu hao waliowateka nyara. Lakini hawakuwasikiliza hao waamuzi wao, maana walifanya uasherati kwa kuifuata miungu mingine, wakajiinamisha mbele yao; wakageuka upesi, na kuiacha njia ile waliyoiendea baba zao, waliozitii amri za BWANA bali wao hawakufanya hivyo. Na wakati BWANA alipowainulia waamuzi, ndipo BWANA alikuwa pamoja na mwamuzi huyo, akawaokoa na mikono ya adui zao siku zote za mwamuzi huyo; maana BWANA alighairi kwa ajili ya kuugua kwao kwa sababu ya watu wale waliowaonea na kuwasumbua. Lakini ikawa, wakati alipokufa mwamuzi huyo, wakarudi nyuma wakafanya maovu kuliko baba zao, kwa kuifuata miungu mingine ili kuitumikia, na kuinama mbele yao; hawakuacha matendo yao, wala njia zao za ukaidi. Basi hasira ya BWANA ikawaka juu ya Israeli, naye akasema, Kwa kuwa taifa hili wamelihalifu agano langu nililowaamuru baba zao, wala hawakuisikiliza sauti yangu; mimi nami tokea sasa sitalifukuza taifa mojawapo la hayo aliyoyaacha Yoshua alipokufa; ili kwa njia ya hayo nipate kuwajaribu Israeli, kwamba wataishika njia ya BWANA kwenda katika njia hiyo, au sivyo. Basi BWANA akawaacha mataifa yale, wala hakuwafukuza kwa upesi, wala hakuwatia katika mikono ya Yoshua.

Soma Amu 2

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha