Isa 53:4-12
Isa 53:4-12 SUV
Hakika ameyachukua masikitiko yetu, Amejitwika huzuni zetu; Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa, Amepigwa na Mungu, na kuteswa. Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona. Sisi sote kama kondoo tumepotea; Kila mmoja wetu amegeukia njia yake mwenyewe; Na BWANA ameweka juu yake Maovu yetu sisi sote. Alionewa, lakini alinyenyekea, Wala hakufunua kinywa chake; Kama mwana-kondoo apelekwaye machinjoni, Na kama vile kondoo anyamazavyo Mbele yao wakatao manyoya yake; Naam, hakufunua kinywa chake. Kwa kuonewa na kuhukumiwa aliondolewa; Na maisha yake ni nani atakayeisimulia? Maana amekatiliwa mbali na nchi ya walio hai; Alipigwa kwa sababu ya makosa ya watu wangu. Wakamfanyia kaburi pamoja na wabaya; Na pamoja na matajiri katika kufa kwake; Ingawa hakutenda jeuri, Wala hapakuwa na hila kinywani mwake. Lakini BWANA aliridhika kumchubua; Amemhuzunisha; Utakapofanya nafsi yake kuwa dhabihu kwa dhambi, Ataona uzao wake, ataishi siku nyingi, Na mapenzi ya BWANA yatafanikiwa mkononi mwake; Ataona mazao ya taabu ya nafsi yake, na kuridhika. Kwa maarifa yake mtumishi wangu mwenye haki Atawafanya wengi kuwa wenye haki; Naye atayachukua maovu yao. Kwa hiyo nitamgawia sehemu pamoja na wakuu, Naye atagawanya nyara pamoja nao walio hodari; Kwa sababu alimwaga nafsi yake hata kufa, Akahesabiwa pamoja na hao wakosao. Walakini alichukua dhambi za watu wengi, Na kuwaombea wakosaji.