Ebr 11:21-26
Ebr 11:21-26 SUV
Kwa imani Yakobo, alipokuwa katika kufa, akambariki kila mmoja wa wana wa Yusufu, akaabudu akiegemea kichwa cha fimbo yake. Kwa imani Yusufu, alipokuwa amekaribia mwisho wake, alitaja habari za kutoka kwao wana wa Israeli, akaagiza kwa habari ya mifupa yake. Kwa imani Musa, alipozaliwa, akafichwa miezi mitatu na wazazi wake, kwa sababu waliona kwamba ni mtoto mzuri; wala hawakuiogopa amri ya mfalme. Kwa imani Musa alipokuwa mtu mzima, akakataa kuitwa mwana wa binti Farao; akaona ni afadhali kupata mateso pamoja na watu wa Mungu kuliko kujifurahisha katika dhambi kwa kitambo; akihesabu ya kuwa kushutumiwa kwake Kristo ni utajiri mkuu kuliko hazina za Misri; kwa kuwa aliyatazamia hayo malipo.