Est 4:8-14
Est 4:8-14 SUV
Pia akampa na nakili ya andiko la mbiu ya kuwaangamiza, iliyotangazwa Shushani, ili amwonyeshe Esta, na kumweleza; tena amwagize aingie kwa mfalme, kumsihi na kuwaombea watu wake. Basi Hathaki akaja, akamwambia Esta maneno ya Mordekai. Ndipo Esta akasema na Hathaki, akamtuma tena kwa Mordekai, kusema, Watumwa wote wa mfalme wanajua sana, hata na watu wa majimbo ya mfalme, ya kwamba mtu ye yote, akiwa mwanamume au mwanamke, atakayemjia mfalme katika ua wa ndani, wala hakuitwa, kuna sheria moja kwake, ni kwamba auawe; isipokuwa yeye ambaye mfalme atamnyoshea fimbo ya dhahabu, ili aishi; wala mimi sikuitwa niingie kwa mfalme yapata siku thelathini. Basi wakamwambia Mordekai maneno ya Esta. Naye Mordekai akawaagiza wampelekee Esta jibu la kusema, Wewe usijidhanie kuwa wewe utaokoka nyumbani mwa mfalme, zaidi ya Wayahudi wote. Kwa maana wewe ukinyamaza kabisa wakati huu, ndipo kutakapowatokea Wayahudi msaada na wokovu kwa njia nyingine; ila wewe utaangamia pamoja na mlango wote wa baba yako; walakini ni nani ajuaye kama wewe hukuujia ufalme kwa ajili ya wakati kama huo?