Mdo 21:1-26
Mdo 21:1-26 SUV
Ikawa tulipokwisha kujitenga nao na kuabiri, tukafika Kosi kwa tanga moja, na siku ya pili yake tukafika Rodo na kutoka huko tukafika Patara, tukapata merikebu itakayovuka mpaka Foinike tukapanda tukatweka. Na tulipoona Kipro tukaiacha upande wa kushoto; tukasafiri mpaka Shamu tukashuka Tiro. Kwa maana huko ndiko merikebu yetu itakakoshusha shehena yake. Tukiisha kuwaona wanafunzi tukakaa huko siku saba, nao wakamwambia Paulo kwa uweza wa Roho asipande kwenda Yerusalemu. Hata tulipotimiza siku zile tukaondoka tukaenda zetu, na watu wote, pamoja na wake zao na watoto wao, wakatusindikiza mpake nje ya mji, tukapiga magoti pwani tukaomba; na baada ya kuagana tukapanda merikebuni, nao wakarudi kwao. Hata tulipomaliza safari yetu kutoka Tiro tukafika Tolemai, tukawaamkua ndugu tukakaa kwao siku moja. Asubuhi yake tukaondoka, tukafika Kaisaria, tukaingia nyumbani mwa Filipo, mhubiri wa Injili, aliyekuwa mmoja wa wale saba, tukakaa kwake. Mtu huyu alikuwa na binti wanne, mabikira, waliokuwa wakitabiri. Basi tulipokuwa tukikaa huko siku nyingi, nabii mmoja jina lake Agabo akashuka kutoka Uyahudi. Alipotufikia akautwaa mshipi wa Paulo, akajifunga miguu na mikono, akasema, Roho Mtakatifu asema hivi, Hivyo ndivyo Wayahudi wa Yerusalemu watakavyomfunga mtu mwenye mshipi huu, nao watamtia katika mikono ya watu wa Mataifa. Basi tuliposikia haya, sisi na watu wa mahali pale, tukamsihi asipande kwenda Yerusalemu. Ndipo Paulo alipojibu, Mnafanya nini, kulia na kunivunja moyo? Kwa maana mimi, licha ya kufungwa, ni tayari hata kuuawa katika Yerusalemu kwa ajili ya jina lake Bwana Yesu. Alipokataa shauri letu, tukanyamaza tukisema, Mapenzi ya Bwana na yatendeke. Baada ya siku zile tukachukua vyombo vyetu tukapanda kwenda Yerusalemu. Baadhi ya wanafunzi wa Kaisaria wakafuatana na sisi, wakamchukua na Mnasoni, mtu wa Kipro, mwanafunzi wa zamani ambaye ndiye tutakayekaa kwake. Tulipofika Yerusalemu wale ndugu wakatukaribisha kwa furaha. Hata siku ya pili yake Paulo akaingia kwa Yakobo pamoja nasi, na wazee wote walikuwako. Na baada ya kuwaamkua, akawaeleza mambo yote moja moja Mungu aliyoyatenda katika Mataifa kwa huduma yake. Nao waliposikia wakamtukuza Mungu, wakamwambia, Ndugu yetu, unaona jinsi Wayahudi walioamini walivyo elfu nyingi, nao wote wana wivu sana kwa ajili ya torati. Nao wameambiwa habari zako, ya kwamba unawafundisha Wayahudi wote wakaao katika Mataifa kumwacha Musa, ukiwaambia wasiwatahiri watoto wao, wala wasizifuate desturi. Basi, ni nini? Bila shaka watasikia kwamba umekuja. Basi fanya neno hili tunalokuambia. Wako kwetu watu wanne waliofungwa na nadhiri. Wachukue watu hao, ujitakase pamoja nao, na kuwagharimia ili wanyoe vichwa vyao, watu wote wapate kujua ya kuwa habari zile walizoambiwa juu yako si kitu, bali wewe mwenyewe unaenenda vizuri na kuishika torati. Lakini kwa habari za watu wa Mataifa walioamini, tuliandika na kutoa hukumu yetu ya wao kujilinda nafsi zao na vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na damu, na kitu kilichosongolewa, na uasherati. Ndipo Paulo akawatwaa wanaume wale, na siku ya pili yake akajitakasa nafsi yake pamoja nao, akaingia ndani ya hekalu, akitangaza habari ya kutimiza siku za utakaso, hata sadaka itolewe kwa ajili ya kila mmoja wao.