2 Sam 22:26-51
2 Sam 22:26-51 SUV
Kwa mtu mwenye fadhili utakuwa mwenye fadhili Kwa mkamilifu utajionyesha kuwa mkamilifu; Kwake ajitakasaye utajionyesha kuwa mtakatifu; Na kwa mpotovu utajionyesha kuwa mkaidi. Na watu wanaoonewa wewe utawaokoa; Ila macho yako ni juu ya wenye kiburi, uwadhili. Kwa kuwa wewe u taa yangu, Ee BWANA; Na BWANA ataniangazia giza langu. Maana kwa msaada wako nafuatia jeshi; Kwa msaada wa Mungu wangu naruka ukuta. Mungu njia yake ni kamilifu; Ahadi ya BWANA imehakikishwa; Yeye ndiye ngao yao Wote wanaomkimbilia. Maana ni nani aliye Mungu, ila BWANA? Ni nani aliye mwamba, ila Mungu wetu? Mungu ndiye ngome yangu yenye nguvu; Naye huwaongoza wakamilifu katika njia yake. Huifanya miguu yangu kuwa kama ya kulungu; Na kunisimamisha mahali pangu pa juu. Ananifundisha mikono yangu vita; Hata mikono yangu yaupinda upinde wa shaba. Nawe umenipa ngao ya wokovu wako; Na unyenyekevu wako umenikuza. Umezifanyizia nafasi hatua zangu, Wala miguu yangu haikuteleza. Nimewafuatia adui zangu, na kuwaangamiza; Wala sikurudi nyuma hata walipokomeshwa. Nami nimewakomesha na kuwapiga-piga wasiweze kusimama; Naam, wameanguka chini ya miguu yangu. Maana umenifunga mshipi wa nguvu kwa vita; Umenitiishia chini yangu walioniondokea. Naam, adui zangu umewafanya wanipe visogo, Ili niwakatilie mbali wanaonichukia. Walitazama, lakini hakuna wa kuokoa; Walimwita BWANA, lakini hakuwajibu. Ndipo nikawaponda kama mavumbi ya nchi, Nikawakanyaga kama matope ya njiani, nikawatawanya. Nawe umeniokoa na mashindano ya watu wangu; Umenihifadhi niwe kichwa cha mataifa; Watu nisiowajua watanitumikia. Wageni watanijia wakinyenyekea; Kwa kusikia tu habari zangu, Mara watanitii. Wageni nao watatepetea, Watatoka katika ngome zao wakitetemeka. BWANA ndiye aliye hai; Na ahimidiwe mwamba wangu; Na atukuzwe Mungu wa mwamba wa wokovu wangu; Naam, Mungu anipatiaye kisasi, Na kuwatweza watu chini yangu, Na kunileta nje nitoke kwa adui zangu; Naam, waniinua juu yao walioniinukia; Waniponya na mtu wa jeuri. Basi, BWANA, nitakushukuru kati ya mataifa, Nami nitaliimbia jina lako. Ampa mfalme wake wokovu mkuu; Amfanyia fadhili masihi wake, Daudi na mzao wake, hata milele.


