Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Samueli 22:26-51 - Compare All Versions

2 Samueli 22:26-51 BHN (Biblia Habari Njema)

“Wewe ni mwaminifu kwa walio waaminifu, mwema kwa wale walio wema. Wewe ni mkamilifu kwa walio wakamilifu, lakini mkatili kwa watu walio waovu. Wewe wawaokoa walio wanyenyekevu, lakini wawaangalia wenye majivuno kuwaporomosha. Ee Mwenyezi-Mungu, wewe u taa yangu, Mungu wangu, unayefukuza giza langu. Kwa msaada wako, wakishambulia kikosi; wewe wanipa nguvu ya kuruka kuta zake. Anachofanya Mungu hakina dosari! Ahadi ya Mwenyezi-Mungu ni ya kuaminika; yeye ni ngao kwa wote wanaomkimbilia. “Nani aliye Mungu isipokuwa Mwenyezi-Mungu? Nani aliye mwamba wa usalama ila Mungu wetu? Mungu huyu ndiye kimbilio langu imara, na ameifanya njia yangu iwe salama. Ameiimarisha miguu yangu kama ya paa, na kuniweka salama juu ya vilele. Hunifunza kupigana vita, mikono yangu iweze kuvuta upinde wa shaba. Umenipa ngao yako ya kuniokoa; msaada wako umenifanya mkuu. Umenirahisishia njia yangu; wala miguu yangu haikuteleza. Niliwafuatia adui zangu na kuwaangamiza, sikurudi nyuma mpaka wameangamizwa. Niliwaangamiza, nikawaangusha chini wasiweze kuinuka tena; walianguka chini ya miguu yangu. Wewe ulinijalia nguvu ya kupigana vita; uliwaporomosha adui chini yangu. Uliwafanya adui zangu wakimbie, na wale walionichukia niliwaangamiza. Walitafuta msaada, lakini hapakuwa na wa kuwaokoa, walimlilia Mwenyezi-Mungu, lakini hakuwajibu. Niliwatwanga na kuwaponda kama mavumbi ya nchi, nikawaponda na kuwakanyaga kama matope barabarani. “Wewe uliniokoa na mashambulizi ya watu wangu, umenifanya mtawala wa mataifa. Watu nisiowajua walinitumikia. Wageni walinijia wakinyenyekea, mara waliposikia habari zangu walinitii. Wageni walikufa moyo; wakaja kutoka ngome zao wakitetemeka. “Mwenyezi-Mungu yu hai! Asifiwe mwamba wangu! Atukuzwe Mungu wangu, mwamba wa wokovu wangu. Yeye ameniwezesha kulipiza kisasi na kuyatiisha mataifa chini yangu. Ameniokoa kutoka adui zangu. Ee Mwenyezi-Mungu, ulinikuza juu ya wapinzani wangu na kunisalimisha mbali na watu wakatili. “Kwa hiyo, nitakutukuza kati ya mataifa, ee Mwenyezi-Mungu, nitaliimbia sifa jina lako. Mungu humjalia mfalme wake ushindi mkubwa; humwonesha fadhili zake huyo aliyemweka wakfu, naam, humfadhili Daudi na wazawa wake milele.”

2 Samueli 22:26-51 SRUV (Swahili Revised Union Version)

Kwa mtu mwenye fadhili utakuwa mwenye fadhili Kwa mkamilifu utajionesha kuwa mkamilifu; Kwake ajitakasaye utajionesha kuwa mtakatifu; Na kwa mpotovu utajionesha kuwa mkaidi. Na watu wanaoonewa wewe utawaokoa; Ila macho yako huwapinga wenye kiburi, uwadhili. Kwa kuwa wewe u taa yangu, Ee BWANA; Na BWANA ataniangazia giza langu. Maana kwa msaada wako nafuatia jeshi; Kwa msaada wa Mungu wangu ninaruka ukuta. Mungu njia yake ni kamilifu; Ahadi ya BWANA imehakikishwa; Yeye ndiye ngao yao Wote wanaomkimbilia. Maana ni nani aliye Mungu, ila BWANA? Ni nani aliye mwamba, ila Mungu wetu? Mungu ndiye ngome yangu yenye nguvu; Naye huwaongoza wakamilifu katika njia yake. Huifanya miguu yangu kuwa kama ya kulungu; Na kunisimamisha mahali pangu pa juu. Ananifundisha mikono yangu vita; Hata mikono yangu inaupanda upinde wa shaba. Nawe umenipa ngao ya wokovu wako; Na unyenyekevu wako umenikuza. Umezifanyia nafasi hatua zangu, Wala miguu yangu haikuteleza. Nimewafuatia adui zangu, na kuwaangamiza; Wala sikurudi nyuma hadi walipokomeshwa. Nami nimewakomesha na kuwapiga wasiweze kusimama; Naam, wameanguka chini ya miguu yangu. Maana umenijaza nguvu ya kupigana vita; Ukawafanya adui zangu wafifie chini yangu. Naam, adui zangu umewafanya wanipe visogo, Ili niwakatilie mbali wanaonichukia. Walitazama, lakini hapakuwa na wa kuwaokoa; Walimwita BWANA, lakini hakuwajibu. Ndipo nikawaponda kama mavumbi ya nchi, Nikawakanyaga kama matope ya njiani, nikawatawanya. Nawe umeniokoa na mashindano ya watu wangu; Umenihifadhi niwe kichwa cha mataifa; Watu nisiowajua watanitumikia. Wageni walinijia wakinyenyekea; Mara tu waliposikia habari zangu, Walinitii. Wageni nao waliishiwa nguvu, Wakatoka katika ngome zao wakitetemeka. BWANA yu hai; Na ahimidiwe mwamba wangu; Na atukuzwe Mungu wangu, mwamba wa wokovu wangu; Naam, Mungu anilipiziaye kisasi, Na kuwatweza watu chini yangu, Na kuniokoa kutoka kwa adui zangu; Naam, waniinua juu yao walioniinukia; Ukaniokoa kutoka kwa watu wajeuri. Basi, BWANA, nitakushukuru kati ya mataifa, Nami nitaliimbia jina lako. Yeye ni mnara wa wokovu kwa mfalme wake; Amfanyia fadhili masihi wake, Kwa Daudi na wazawa wake, hata milele.

2 Samueli 22:26-51 SUV (Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia)

Kwa mtu mwenye fadhili utakuwa mwenye fadhili Kwa mkamilifu utajionyesha kuwa mkamilifu; Kwake ajitakasaye utajionyesha kuwa mtakatifu; Na kwa mpotovu utajionyesha kuwa mkaidi. Na watu wanaoonewa wewe utawaokoa; Ila macho yako ni juu ya wenye kiburi, uwadhili. Kwa kuwa wewe u taa yangu, Ee BWANA; Na BWANA ataniangazia giza langu. Maana kwa msaada wako nafuatia jeshi; Kwa msaada wa Mungu wangu naruka ukuta. Mungu njia yake ni kamilifu; Ahadi ya BWANA imehakikishwa; Yeye ndiye ngao yao Wote wanaomkimbilia. Maana ni nani aliye Mungu, ila BWANA? Ni nani aliye mwamba, ila Mungu wetu? Mungu ndiye ngome yangu yenye nguvu; Naye huwaongoza wakamilifu katika njia yake. Huifanya miguu yangu kuwa kama ya kulungu; Na kunisimamisha mahali pangu pa juu. Ananifundisha mikono yangu vita; Hata mikono yangu yaupinda upinde wa shaba. Nawe umenipa ngao ya wokovu wako; Na unyenyekevu wako umenikuza. Umezifanyizia nafasi hatua zangu, Wala miguu yangu haikuteleza. Nimewafuatia adui zangu, na kuwaangamiza; Wala sikurudi nyuma hata walipokomeshwa. Nami nimewakomesha na kuwapiga-piga wasiweze kusimama; Naam, wameanguka chini ya miguu yangu. Maana umenifunga mshipi wa nguvu kwa vita; Umenitiishia chini yangu walioniondokea. Naam, adui zangu umewafanya wanipe visogo, Ili niwakatilie mbali wanaonichukia. Walitazama, lakini hakuna wa kuokoa; Walimwita BWANA, lakini hakuwajibu. Ndipo nikawaponda kama mavumbi ya nchi, Nikawakanyaga kama matope ya njiani, nikawatawanya. Nawe umeniokoa na mashindano ya watu wangu; Umenihifadhi niwe kichwa cha mataifa; Watu nisiowajua watanitumikia. Wageni watanijia wakinyenyekea; Kwa kusikia tu habari zangu, Mara watanitii. Wageni nao watatepetea, Watatoka katika ngome zao wakitetemeka. BWANA ndiye aliye hai; Na ahimidiwe mwamba wangu; Na atukuzwe Mungu wa mwamba wa wokovu wangu; Naam, Mungu anipatiaye kisasi, Na kuwatweza watu chini yangu, Na kunileta nje nitoke kwa adui zangu; Naam, waniinua juu yao walioniinukia; Waniponya na mtu wa jeuri. Basi, BWANA, nitakushukuru kati ya mataifa, Nami nitaliimbia jina lako. Ampa mfalme wake wokovu mkuu; Amfanyia fadhili masihi wake, Daudi na mzao wake, hata milele.

2 Samueli 22:26-51 NEN (Neno)

“Kwa yeye aliye mwaminifu unajionesha kuwa mwaminifu, kwa asiye na hatia unajionesha kutokuwa na hatia, kwa aliye mtakatifu unajionesha kuwa mtakatifu, lakini kwa aliyepotoka unajionesha kuwa mkaidi. Wewe huwaokoa wanyenyekevu, lakini macho yako ni juu ya wenye kiburi ili uwashushe. Wewe ni taa yangu, Ee BWANA. BWANA hulifanya giza langu kuwa mwanga. Kwa msaada wako naweza kushinda jeshi, nikiwa pamoja na Mungu wangu nitaweza kuruka ukuta. “Kuhusu Mungu, njia yake ni kamilifu; neno la BWANA halina dosari. Yeye ni ngao kwa wote wanaokimbilia kwake. Kwa maana ni nani aliye Mungu zaidi ya BWANA? Ni nani aliye Mwamba isipokuwa Mungu wetu? Mungu ndiye anivikaye nguvu, na kufanya njia yangu kuwa kamilifu. Huifanya miguu yangu kama miguu ya kulungu, huniwezesha kusimama mahali palipo juu. Huifundisha mikono yangu kupigana vita; mikono yangu inaweza kupinda upinde wa shaba. Hufanya msaada wa wokovu wako kuwa ngao yangu; msaada wako umeniinua niwe mkuu. Huyapanua mapito yangu, ili miguu yangu isiteleze. “Niliwafuatia adui zangu na nikawaseta, sikurudi nyuma hadi walipoangamizwa. Niliwaseta kabisa, nao hawakuweza kuinuka tena; walianguka chini ya miguu yangu. Ulinivika nguvu kwa ajili ya kupigana vita; uliwafanya adui zangu wasujudu miguuni pangu. Uliwafanya adui zangu wageuke na kukimbia, nami nikawaangamiza adui zangu. Walipiga yowe, lakini hapakuwa na yeyote wa kuwaokoa; walimlilia BWANA, lakini hakuwajibu. Niliwaponda kama mavumbi ya nchi; niliwaponda na kuwakanyaga kama tope barabarani. “Umeniokoa kutokana na mashambulizi ya watu wangu; umenihifadhi mimi kama kiongozi wa mataifa. Watu ambao sikuwajua wananitumikia, nao wageni huja wakininyenyekea, mara wanisikiapo, hunitii. Wote wanalegea, wanatoka katika ngome zao wakitetemeka. “BWANA yu hai! Sifa ni kwa Mwamba wangu! Atukuzwe Mungu, Mwamba, Mwokozi wangu! Yeye ndiye Mungu anilipiziaye kisasi, ayawekaye mataifa chini yangu, aniwekaye huru toka kwa adui zangu. Uliniinua juu ya adui zangu; uliniokoa toka kwa watu wajeuri. Kwa hiyo nitakusifu, Ee BWANA, kati ya mataifa; nitaliimbia sifa jina lako. “Humpa mfalme wake ushindi mkuu; huonesha fadhili zake kwa mpakwa mafuta wake, kwa Daudi na wazao wake milele.”