Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Pet UTANGULIZI

UTANGULIZI
Mwandishi wa Waraka huu ambaye anajitambulisha kama Simoni Petro, “mtumwa na mtume wa Yesu Kristo” (1:1) anatamka wazi kwamba alishuhudia kwa macho yake mwenyewe tukio lile la Yesu kubadilika sura (1:16-18) na kwamba yeye alikuwa mwandishi wa Waraka uliotangulia huu wa sasa (3:1). Mji au mahali Waraka huu ulipopelekwa hautajwi wala walengwa wake hawatajwi. Kwa sababu hiyo inakubalika kwamba uliandikwa kwa ajili ya jumuiya zote za kanisa (tazama utangulizi kwa Waraka wa Kwanza wa Petro).
Waraka huu, tofauti na ule wa kwanza, una mawazo mengi mengi kutoka Agano la Kale hata kama hayo hayakunukuliwa moja kwa moja (2 Pet 2:5-7, rejea Mwa 6:1-7,24 na 19:1-16,24; 2 Pet 2:15-16; Hes 22:4-35; 2 Pet 2:22; Mit 26:11; 2 Pet 3:5; Mwa 1:6-8; 2 Pet 3:6; Mwa 7:11; 2 Pet 3:8; Zab 90:4; 2 Pet 3:13; Isa 65:17 na 66:22).
Waraka wenyewe unaanza, kama kawaida ya Nyaraka za Agano Jipya, na salamu (1:1-2) kisha kuna mwito kwa walengwa kufikiri juu ya “ahadi kubwa mno za thamani” ambazo waumini walipewa ili wapate “kuwa washirika wa tabia ya Uungu” (1:4). Tena, mwandishi anawaambia hao waumini wajitahidi zaidi “kufanya imara kuitwa kwenu na uteule wenu… Maana hivi mtaruzukiwa kwa ukarimu kuingia katika ufalme wa milele wa Bwana wetu, Mwokozi wetu Yesu Kristo.” (1:10-11). Kisha Petro anawatia moyo wasomaji wake kwa kutaja msingi wa “neno la unabii lililo imara zaidi… kama taa ing’aayo mahali penye giza”, ambalo itakuwa vema kama wakilizingatia (1:19-21). Kutokana na hilo mwandishi anashutumu vikali mafundisho na mwenendo wa manabii na waalimu wa uongo ambao wanawaongoza watu wa Mungu katika makosa “wakimkana hata Bwaba aliyewanunua” (2:1). Kutokana na wazo hili la mwisho, sura yote ya 2 inaendelea kushutumu mafundisho mapotovu na karibu sura yote imepangwa kwa mfano wa Waraka wa Yuda na sehemu zake sambamba zinaweza kuonekana kwa msomaji.
Sura ya 3 inashughulikia tatizo moja lililowakabili waumini wa nyakati hizo, yaani kukawia kurudi kwake Bwana. Kukawia huko kuliwafanya wengi kukata tamaa. Ili kuwatia moyo, mwandishi anawakumbusha kwamba vipimo vya wakati vya binadamu si sawa na vipimo vya Bwana (3:8,10,13-14); na kwamba Yesu Kristo ambaye Wakristo na kanisa lote wanamwamini ni ufunguo kamili wa fumbo la kuweko kwetu na mpango wa milele wa ukombozi wa binadamu (3:8-9,15).

Iliyochaguliwa sasa

2 Pet UTANGULIZI: SUV

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha