Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Nya 18:8-27

2 Nya 18:8-27 SUV

Ndipo mfalme wa Israeli akamwita akida mmoja, akasema, Mlete hima Mikaya mwana wa Imla. Basi, mfalme wa Israeli na Yehoshafati mfalme wa Yuda walikuwa wamekaa kila mtu katika kiti chake cha enzi, wamevaa mavazi yao, wakikaa penye sakafu pa kuingilia lango la Samaria; nao manabii wote wakafanya unabii mbele yao. Na Zedekia mwana wa Kenaana akajifanyia pembe za chuma, akasema, BWANA asema hivi, Kwa hizi utawasukuma Washami, hata watakapoangamia. Na manabii wote wakatoa unabii huo, wakisema, Kwea Ramoth-gileadi, ukafanikiwe, kwa kuwa BWANA atautia mkononi mwa mfalme. Na yule mjumbe, aliyekwenda kumwita Mikaya, akamwambia, akasema, Angalia, maneno ya manabii kwa kinywa kimoja yasema mema kwa mfalme; neno lako basi na liwe kama mojawapo lao, ukaseme mema. Mikaya akasema, Kama aishivyo BWANA, neno lile atakalolinena Mungu wangu, ndilo nitakalolinena. Na alipokuja kwa mfalme, mfalme akamwambia, Je! Mikaya, tuende Ramoth-gileadi vitani, au niache? Akasema, Kweeni, mkafanikiwe; nao watatiwa mikononi mwenu. Mfalme akamwambia, Mara ngapi nikuapishe, usiniambie neno ila yaliyo kweli, kwa jina la BWANA? Akasema, Naliwaona Waisraeli wote wametawanyika milimani, kama kondoo wasio na mchungaji; BWANA akasema, Hawa hawana bwana; na warudi kila mtu nyumbani kwake kwa amani. Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, Je! Sikukuambia, hatanibashiria mema, ila mabaya? Mikaya akasema, Sikieni basi neno la BWANA; Nalimwona BWANA ameketi katika kiti chake cha enzi na jeshi lote la mbinguni wamesimama mkono wake wa kuume na wa kushoto. BWANA akasema, Ni nani atakayemdanganya Ahabu mfalme wa Israeli, ili akwee Ramoth-gileadi akaanguke? Basi huyu akasema hivi; na huyu hivi. Akatoka pepo, akasimama mbele za BWANA, akasema, Mimi nitamdanganya. BWANA akamwambia, Jinsi gani? Akasema, Nitaondoka, na kuwa pepo wa uongo vinywani mwa manabii wake wote. Akasema, Utamdanganya, na kudiriki pia; ondoka, ukafanye hivyo. Basi sasa, angalia, BWANA ametia pepo wa uongo vinywani mwa manabii wako hawa; naye BWANA amenena mabaya juu yako. Ndipo akakaribia Zedekia mwana wa Kenaana, akampiga Mikaya kofi la shavu, akasema, Alitokaje kwangu roho ya BWANA ili aseme na wewe? Mikaya akasema, Angalia utaona siku ile, utakapoingia katika chumba cha ndani ili ujifiche. Mfalme wa Israeli akasema, Mchukueni Mikaya mkamrudishe kwa Amoni mkuu wa mji, na kwa Yoashi mwana wa mfalme; mkaseme, Mfalme asema hivi, Mtieni huyu gerezani, mkamlishe chakula cha shida, na maji ya shida, hata nitakaporudi kwa amani. Mikaya akasema, Ukirudi kabisa kwa amani, BWANA hakusema kwa mimi. Akasema, Sikieni, enyi watu wote.

Soma 2 Nya 18

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha