Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Fal 22:8-28

1 Fal 22:8-28 SUV

Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, Yupo mtu mmoja, ambaye tungeweza kumwuliza BWANA kwa yeye, yaani Mikaya mwana wa Imla; lakini namchukia; kwa sababu hanibashirii mema, ila mabaya. Yehoshafati akasema, La! Mfalme asiseme hivi. Ndipo mfalme wa Israeli akamwita akida, akamwambia, mlete hima Mikaya mwana wa Imla. Basi mfalme wa Israeli na Yehoshafati mfalme wa Yuda walikuwa wakikaa kila mtu katika kiti chake cha enzi, wamevaa mavazi yao, katika sakafu langoni pa Samaria; na manabii wote wakafanya unabii mbele yao. Na Zedekia mwana wa Kenaana akajifanyia pembe za chuma, akasema, BWANA asema hivi, Kwa hizo utawasukuma Washami, hata waharibike. Na manabii wote wakasema hivyo kwa unabii, wakisema, Kwea Ramoth-Gileadi, ukafanikiwe; kwa kuwa BWANA atautia mkononi mwa mfalme. Na yule mjumbe, aliyekwenda kumwita Mikaya, akamwambia, akasema, Angalia sasa, maneno ya manabii kwa kinywa kimoja husema mema kwa mfalme; neno lako na liwe, nakusihi, kama neno la mmojawapo wao, ukaseme mema. Mikaya akasema, Kama BWANA aishivyo, neno lile BWANA aniambialo, ndilo nitakalolinena. Na alipokuja kwa mfalme, mfalme alimwambia, Je! Mikaya, tuende Ramoth-Gileadi kupiga vita, au tunyamaze? Akamwambia, Kwea, ufanikiwe; kwa kuwa BWANA atautia mkononi mwa mfalme. Mfalme akamwambia, Mara ngapi nikuapishe usiniambie neno ila yaliyo kweli, kwa jina la BWANA? Akasema, Naliwaona Waisraeli wote wametawanyika milimani, kama kondoo wasio na mchungaji. BWANA akasema, Hawa hawana bwana; na warudi kila mtu nyumbani kwake kwa amani. Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, Je! Sikukuambia, hatanibashiria mema, ila mabaya? Mikaya akasema, Sikia basi neno la BWANA; Nalimwona BWANA ameketi katika kiti chake cha enzi, na jeshi lote la mbinguni wamesimama upande wa mkono wake wa kuume na wa kushoto. BWANA akasema, Ni nani atakayemdanganya Ahabu, ili akwee Ramoth-Gileadi akaanguke? Basi huyu akasema hivi; na huyu hivi. Akatoka pepo, akasimama mbele za BWANA, akasema, Mimi nitamdanganya. BWANA akamwambia, Jinsi gani? Akasema, Nitaondoka, na kuwa pepo wa uongo kinywani mwa manabii wake wote. Akasema, Utamdanganya, na kudiriki pia; ondoka ukafanye hivyo. Basi angalia, BWANA ametia pepo wa uongo kinywani mwa manabii wako hawa wote; naye BWANA amenena mabaya juu yako. Ndipo akakaribia Zedekia, mwana wa Kenaana, akampiga Mikaya kofi la shavu, akasema, Roho ya BWANA alitokaje kwangu ili aseme na wewe? Mikaya akamwambia, Angalia, utaona siku ile utakapoingia katika chumba cha ndani ili ujifiche. Mfalme wa Israeli akasema, Mchukueni Mikaya, mkamrudishe kwa Amoni mkuu wa mji na kwa Yoashi mwana wa mfalme; mkaseme, Mfalme asema hivi, Mtieni mtu huyu gerezani, mkamlishe kwa chakula cha shida, na maji ya shida, hata nitakaporudi kwa amani. Mikaya akasema, Ukirudi kabisa kwa amani, BWANA hakusema kwa mimi. Akasema, Sikieni, enyi watu wote.

Soma 1 Fal 22

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na 1 Fal 22:8-28

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha