Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Fal 18:30-46

1 Fal 18:30-46 SUV

Kisha Eliya akawaambia watu wote, Nikaribieni mimi. Watu wote wakamkaribia. Akaitengeneza madhabahu ya BWANA iliyovunjika. Eliya akatwaa mawe kumi na mawili, kwa hesabu ya kabila za wana wa Yakobo, aliyejiliwa na neno la BWANA na kuambiwa, Jina lako litakuwa Israeli. Naye akaijenga madhabahu kwa mawe hayo katika jina la BWANA; akafanya mfereji, kama wa vipimo viwili vya mbegu, ukiizunguka madhabahu. Kisha akazipanga zile kuni, akamkata yule ng’ombe vipande vipande, akaviweka juu ya kuni. Akasema, Jazeni mapipa manne maji, mkayamwage juu ya sadaka ya kuteketezwa, na juu ya kuni. Akasema, Fanyeni mara ya pili. Wakafanya mara ya pili. Akasema, Fanyeni mara ya tatu. Wakafanya mara ya tatu. Yale maji yakaizunguka madhabahu; akaujaza mfereji maji. Ikawa, wakati wa kutoa dhabihu ya jioni, Eliya nabii akakaribia, akasema, Ee BWANA, Mungu wa Ibrahimu, na wa Isaka, na wa Israeli, na ijulikane leo ya kuwa wewe ndiwe Mungu katika Israeli, na ya kuwa mimi ni mtumishi wako, na ya kuwa nimefanya mambo haya yote kwa neno lako. Unisikie, Ee BWANA, unisikie, ili watu hawa wajue ya kuwa wewe, BWANA, ndiwe Mungu, na ya kuwa wewe umewageuza moyo wakurudie. Ndipo moto wa BWANA ukashuka, ukaiteketeza sadaka ya kuteketezwa, na kuni, na mawe, na mavumbi, ukayaramba yale maji yaliyokuwamo katika mfereji. Na watu wote walipoona, wakaanguka kifudifudi; wakasema, BWANA ndiye Mungu, BWANA ndiye Mungu. Eliya akawaambia, Wakamateni hao manabii wa Baali, asiokoke hata mmoja. Wakawakamata; na Eliya akawachukua mpaka kijito cha Kishoni, akawaua huko. Naye Eliya akamwambia Ahabu, Haya! Inuka, ule, unywe; kwani pana sauti ya mvua tele. Basi Ahabu akainuka ili ale na kunywa. Naye Eliya akapanda juu mpaka kilele cha Karmeli; akasujudu kifudifudi, akainama uso mpaka magotini. Akamwambia mtumishi wake, Kwea sasa, utazame upande wa bahari. Akakwea, akatazama, na kusema, Hakuna kitu. Naye akanena, Enenda tena mara saba. Ikawa mara ya saba akasema, Tazama, wingu linatoka katika bahari, nalo ni dogo kama mkono wa mtu. Akanena, Enenda, umwambie Ahabu, Tandika, ushuke, mvua isikuzuie. Ikawa, muda si muda, mbingu zikawa nyeusi kwa mawingu na upepo, ikanyesha mvua nyingi. Ahabu akapanda garini, akaenda zake Yezreeli. Mkono wa BWANA ulikuwa juu ya Eliya; akajikaza viuno, akapiga mbio mbele ya Ahabu mpaka kuiingia Yezreeli.

Soma 1 Fal 18

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha