Warumi 4:13-22
Warumi 4:13-22 NENO
Kwa maana ile ahadi kwamba angeurithi ulimwengu haikuja kwa Abrahamu au kwa wazao wake kupitia kwa sheria bali kupitia kwa haki ipatikanayo kwa imani. Kwa maana ikiwa wale wanaoishi kwa sheria ndio warithi, imani haina thamani na ahadi haifai kitu, kwa sababu sheria huleta ghadhabu. Mahali ambapo hakuna sheria, hakuna makosa. Kwa hiyo, ahadi huja kupitia kwa imani, ili iwe ni kwa neema, na ihakikishiwe wazao wote wa Abrahamu, si kwa wale walio wa sheria peke yao, bali pia kwa wale walio wa imani ya Abrahamu. Yeye ndiye baba yetu sisi sote. Kama ilivyoandikwa: “Nimekufanya wewe kuwa baba wa mataifa mengi.” Yeye ni baba yetu mbele za Mungu, ambaye yeye alimwamini, yule Mungu anayefufua waliokufa, na kuvitaja vitu ambavyo haviko kana kwamba viko. Akitarajia yasiyoweza kutarajiwa, Abrahamu akaamini, akawa baba wa mataifa mengi, kama alivyoahidiwa kwamba, “Hivyo ndivyo uzao wako utakavyokuwa.” Abrahamu hakuwa dhaifu katika imani hata alipofikiri hali ya mwili wake, ambao ulikuwa kama uliokufa, kwani umri wake ulikuwa unakaribia miaka mia moja, au alipofikiri hali ya kufa ya tumbo la Sara. Lakini Abrahamu hakusitasita kwa kutokuamini ahadi ya Mungu, bali alitiwa nguvu katika imani yake na kumpa Mungu utukufu, akiwa na hakika kabisa kwamba Mungu alikuwa na uwezo wa kutimiza lile aliloahidi. Hii ndio sababu, “ilihesabiwa kwake kuwa haki.”