Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Warumi 10:5-21

Warumi 10:5-21 NENO

Musa anaandika kuhusu haki ile itokanayo na sheria, kwamba, “Mtu atendaye matendo hayo ataishi kwa hayo.” Lakini ile haki itokanayo na imani husema hivi: “Usiseme moyoni mwako, ‘Ni nani atakayepanda mbinguni?’” (yaani ili kumleta Kristo chini) “au ‘Ni nani atashuka kwenda Kuzimu?’” (yaani ili kumleta Kristo kutoka kwa wafu). Lakini andiko lasemaje? “Lile neno liko karibu nawe, liko kinywani mwako na moyoni mwako,” yaani lile neno la imani tunalolihubiri. Kwa sababu, ukikiri kwa kinywa chako kwamba “Yesu ni Bwana,” na kuamini moyoni mwako kwamba Mungu alimfufua kutoka kwa wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini na hivyo kuhesabiwa haki, tena kwa kinywa mtu hukiri na hivyo kupata wokovu. Kama Maandiko yanavyosema, “Yeyote amwaminiye hataaibika kamwe.” Kwa maana hakuna tofauti kati ya Myahudi na mtu wa Mataifa, yeye ni Bwana wa wote, mwenye utajiri kwa wote wamwitao. Kwa maana, “Kila mtu atakayeliitia Jina la Bwana, ataokolewa.” Lakini watamwitaje yeye ambaye hawajamwamini? Nao watawezaje kumwamini yeye ambaye hawajamsikia? Tena watamsikiaje bila mtu kuwahubiria? Nao watahubirije wasipopelekwa? Kama ilivyoandikwa, “Tazama jinsi ilivyo mizuri miguu yao wale wanaohubiri Habari Njema!” Lakini si wote waliotii Habari Njema. Kwa maana Isaya asema, “Bwana, ni nani aliyeamini ujumbe wetu?” Basi, imani chanzo chake ni kusikia, na kusikia huja kwa neno la Kristo. Lakini nauliza: Je, wao hawakusikia? Naam, wamesikia, kwa maana: “Sauti yao imeenea duniani pote, nayo maneno yao yameenea hadi miisho ya ulimwengu.” Nami nauliza tena: Je, Waisraeli hawakuelewa? Kwanza, Musa asema, “Nitawafanya mwe na wivu kwa watu wale ambao si taifa. Nitawakasirisha kwa taifa lile lisilo na ufahamu.” Naye Isaya kwa ujasiri mwingi anasema, “Nimeonekana na watu wale ambao hawakunitafuta. Nilijifunua kwa watu wale ambao hawakunitafuta.” Lakini kuhusu Israeli anasema, “Mchana kutwa nimewanyooshea watu wakaidi na wasiotii mikono yangu.”

Video ya Warumi 10:5-21