Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi Utangulizi

Utangulizi
Jina la kitabu hiki kwa Kiebrania ni “Sepher Tehillim”, ambalo maana yake ni “Nyimbo za Sifa.” Jina la Kiyunani ni “Psalmoi” yaani “Nyimbo zinazoimbwa kwa kutumia ala za muziki za nyuzi” na ndiyo kiini cha kitabu hiki. Kitabu hiki kina sura mia moja na hamsini, na sura nyingi zinajitosheleza, isipokuwa chache tu. Zaburi ya mwisho (150) ni wimbo wa sifa, kuonesha kuwa kilele cha kitabu kizima ni wimbo wa sifa.
Zaburi zilitungwa kwa mvuto wa hali ya juu na wa kusisimua sana na hivyo huwa zinaleta msisimko wa pekee. Kwa kuwa zilitungwa kutokana na uzoefu wa maisha kutoka mazingira na nyakati mbalimbali, bado zimekuwa na mvuto mkubwa ulimwenguni kote kwa miaka mingi tangu ziandikwe.
Mara kwa mara, Zaburi zimeainishwa kwa kufuata namna fulani za maelezeo au mafundisho. Aina mbalimbali za zaburi hizo ni kama vile zile zilizohusu sala ya shukrani na sifa, maombolezo, nyimbo za kuonesha tumaini kwa Mungu, toba, kusimika au kutawaza viongozi, kuhusu Masiya, historia ya uumbaji, na zilizohusu hekima ya jinsi binadamu anavyopaswa kutunza mahusiano mema na Mungu na jirani yake.
Inaaminika kwamba makusanyo ya awali yalifanywa na Daudi. Nyongeza nyingine na mpangilio inawezekana vilifanywa na Sulemani, Yehoshafati, Hezekia, Yosia na wengine.
Waandishi
Inaaminiwa kuwa kitabu cha Zaburi ni matokeo ya kazi ya watu wengi, wakiwemo: Daudi (73), Asafu (12), Wana wa Kora (10), Musa (1), Hemani (1), Ethani (1), na Sulemani (2). Waandishi wa Zaburi hamsini hawajulikani.
Kusudi
Kuelezea umuhimu wa mashairi katika sifa, kuabudu na kukiri dhambi mbele za Mungu.
Mahali
Palestina na Babeli.
Tarehe
Kati ya wakati wa Musa (1440 K.K.) na wakati wa utumwa wa Babeli (586 K.K.).
Wahusika Wakuu
Daudi, Asafu, Wana wa Kora, Musa, Hemani na Sulemani.
Wazo Kuu
Kusifu ni kutambua na kutangaza ukuu wa Mungu, kufurahia na kudhihirisha wema wake.
Mambo Muhimu
Zaburi zimeelezea ufunuo wa Mungu, uumbaji, hali ya mwanadamu, wokovu, dhambi na uovu, toba, haki na uadilifu, kuabudu na kusifu, maombi na hukumu.
Yaliyomo
Kitabu cha kwanza: 1–41
Kitabu cha pili: 42–72
Kitabu cha tatu: 73–89
Kitabu cha nne: 90–106
Kitabu cha tano: 107–150.

Iliyochaguliwa sasa

Zaburi Utangulizi: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia