Zaburi 77
77
Zaburi 77
Matendo makuu ya Mungu yanakumbukwa
Kwa mwimbishaji. Mtindo wa Yeduthuni. Zaburi ya Asafu.
1 Nilimlilia Mungu ili anisaidie,
nilimlilia Mungu ili anisikie.
2 Nilipokuwa katika taabu, nilimtafuta Bwana,
usiku nilinyoosha mikono bila kuchoka
na nafsi yangu ilikataa kufarijika.
3 Ee Mungu, nilikukumbuka wewe, nikalia kwa huzuni;
nikatafakari, roho yangu ikadhoofika.
4 Ulizuia macho yangu kufumba;
nilikuwa nasumbuka, nikashindwa kusema.
5 Nilitafakari kuhusu siku zilizopita,
miaka mingi iliyopita,
6nilikumbuka nilivyoimba nyimbo usiku.
Moyo wangu ulitafakari
na roho yangu ikauliza:
7 “Je, Bwana atakataa milele?
Je, hatatenda mema tena?
8 Je, upendo wake usio na mwisho umetoweka milele?
Je, ahadi yake imekoma nyakati zote?
9 Je, Mungu amesahau kuwa na huruma?
Je, katika hasira amezuia fadhili zake?”
10 Ndipo nikawaza, “Huu ndio udhaifu wangu:
lakini nitakumbuka
miaka ya mkono wa kuume
wa Aliye Juu Sana.”
11 Nitayakumbuka matendo ya Bwana;
naam, nitaikumbuka miujiza yako ya zamani.
12 Nitazitafakari kazi zako zote
na kuyawaza matendo yako makuu.
13 Ee Mungu, njia zako ni takatifu.
Ni mungu yupi aliye mkuu kama Mungu wetu?
14 Wewe ndiwe Mungu utendaye miujiza,
umeonesha uwezo wako kati ya mataifa.
15 Kwa mkono wako wenye nguvu umewakomboa watu wako,
uzao wa Yakobo na Yusufu.
16 Maji yalikuona, Ee Mungu,
maji yalikuona yakakimbia,
vilindi vilitetemeka.
17 Mawingu yalimwaga maji,
mbingu zikatoa ngurumo kwa radi;
mishale yako ilimetameta huku na huko.
18 Ngurumo yako ilisikika katika upepo wa kisulisuli,
umeme wako wa radi ukaangaza dunia,
nchi ikatetemeka na kutikisika.
19 Njia yako ilipita baharini,
mapito yako kwenye maji makuu,
ingawa nyayo zako hazikuonekana.
20 Uliongoza watu wako kama kundi
kwa mkono wa Musa na Haruni.
Iliyochaguliwa sasa
Zaburi 77: NEN
Kuonyesha
Nakili
Linganisha
Shirikisha
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Holy Bible, Kiswahili Contemporary Version™ (Neno: Biblia Takatifu™) | Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. | Used with permission. All rights reserved worldwide.
Biblica® Cross Reference System | Copyright © 2025 by Biblica, Inc. | Used with permission. All rights reserved worldwide.