Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 73

73
KITABU CHA TATU
(Zaburi 73–89)
Zaburi 73
Haki Ya Mungu
Zaburi ya Asafu.
1 Hakika Mungu ni mwema kwa Israeli,
kwa wale ambao mioyo yao ni safi.
2 Bali kwangu mimi, miguu yangu ilikuwa karibu kuteleza;
nilikuwa karibu mguu wangu kuachia uliposimama.
3 Kwa maana niliwaonea wivu wenye kujivuna
nilipoona kufanikiwa kwa waovu.
4Wao hawana taabu,#73:4 Tafsiri nyingine zinasema: hawana maumivu katika kufa kwao.
miili yao ina afya na nguvu.
5 Hawapati shida zinazowataabisha watu wengine,
wala hawapati mapigo kama wanadamu wengine.
6 Kwa hiyo kiburi ni mkufu wao,
wamejivika jeuri.
7 Uovu hutoka katika mioyo yao iliyokufa ganzi,
majivuno maovu kutoka mioyoni mwao hauna kikomo.
8 Hudhihaki na kusema kwa ukorofi,
katika majivuno yao wanatishia kutesa.
9 Vinywa vyao huweka madai hata kwa mbingu,
nazo ndimi zao humiliki duniani.
10Kwa hiyo watu wao huwageukia
na kunywa maji tele.#73:10 Au: na kupokea yote wasemayo.
11 Wanasema, “Mungu awezaje kujua?
Je, Yeye Aliye Juu Sana anayo maarifa?”
12 Hivi ndivyo walivyo waovu:
siku zote hawajali,
wanaongezeka katika utajiri.
13 Hakika nimeuweka moyo wangu safi bure,
ni bure nimenawa mikono yangu nisiwe na hatia.
14 Mchana kutwa nimetaabika,
nimeadhibiwa kila asubuhi.
15Kama ningesema, “Nitasema hivi,”
ningelikuwa nimewasaliti watoto wako.
16 Nilipojaribu kuelewa haya yote,
yalikuwa magumu kwangu kuelewa.
17 Mpaka nilipoingia patakatifu pa Mungu,
ndipo nilipotambua mwisho wao.
18 Hakika unawaweka mahali pa utelezi,
unawaangusha chini kwa uharibifu.
19 Tazama jinsi wanavyoangamizwa ghafula,
wanatoweshwa kabisa na vitisho!
20 Kama ndoto mtu aamkapo,
hivyo wakati uinukapo, Ee Bwana,
utawatowesha kama ndoto.
21Wakati moyo wangu ulipohuzunishwa,
na roho yangu ilipotiwa uchungu,
22 nilikuwa mpumbavu na mjinga,
nilikuwa mnyama mkatili mbele yako.
23 Hata hivyo niko pamoja nawe siku zote,
umenishika mkono wangu wa kuume.
24 Unaniongoza kwa shauri lako,
hatimaye utaniingiza katika utukufu.
25 Nani niliye naye mbinguni ila wewe?
Dunia haina chochote ninachokitamani ila wewe.
26 Mwili na moyo wangu vyaweza kushindwa,
bali Mungu ni nguvu ya moyo wangu
na fungu langu milele.
27 Wale walio mbali nawe wataangamia,
unawaangamiza wote wasio waaminifu kwako.
28 Lakini kwangu mimi,
ni vyema kuwa karibu na Mungu.
Nimemfanya Bwana Mwenyezi kimbilio langu;
nami nitayasimulia matendo yako yote.

Iliyochaguliwa sasa

Zaburi 73: NEN

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha