Zaburi 144
144
Zaburi 144
Mfalme amshukuru Mungu kwa ushindi
Zaburi ya Daudi.
1Ahimidiwe Bwana Mwamba wangu,
aifundishaye mikono yangu vita,
na vidole vyangu kupigana.
2Yeye ni Mungu wangu wa upendo na ulinzi wangu,
ngome yangu na mwokozi wangu,
ngao yangu, ninayemkimbilia,
ambaye huwatiisha mataifa chini yangu.
3Ee Bwana, mwanadamu ni nini hata umjali,
Binadamu ni nini hata umfikirie?
4Mwanadamu ni kama pumzi,
siku zake ni kama kivuli kinachopita.
5Ee Bwana, pasua mbingu zako, ushuke,
gusa milima ili itoe moshi.
6Peleka umeme uwatawanye adui,
lenga mishale yako uwashinde.
7Nyoosha mkono wako kutoka juu,
nikomboe na kuniokoa
kutoka maji makuu,
kutoka mikononi mwa wageni
8ambao vinywa vyao vimejaa uongo,
na mikono yao ya kuume ni midanganyifu.
9Ee Mungu, nitakuimbia wimbo mpya,
kwa zeze yenye nyuzi kumi nitakuimbia,
10kwa Yule awapaye wafalme ushindi,
ambaye humwokoa Daudi, mtumishi wake,
kutokana na upanga hatari.
11Nikomboe na uniokoe
kutoka mikononi mwa wageni
ambao vinywa vyao vimejaa uongo,
na mikono yao ya kuume ni midanganyifu.
12Kisha wana wetu wakati wa ujana wao
watakuwa kama mimea iliyotunzwa vizuri,
binti zetu watakuwa kama nguzo zilizoviringwa
kurembesha jumba la kifalme.
13Ghala zetu zitajazwa
aina zote za mahitaji.
Kondoo wetu watazaa kwa maelfu,
kwa makumi ya maelfu katika mashamba yetu;
14maksai wetu watakokota
mizigo mizito.
Hakutakuwa na kubomoka kuta,
hakuna kuchukuliwa mateka,
wala kilio cha taabu
katika barabara zetu.
15Heri watu ambao hili ni kweli;
heri wale ambao Bwana ni Mungu wao.
Iliyochaguliwa sasa
Zaburi 144: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Biblia Takatifu™ Neno™
Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Version™
Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.