Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 118

118
Zaburi 118
Shukrani kwa ajili ya ushindi
1 Mshukuruni Bwana, kwa kuwa ni mwema;
fadhili zake zadumu milele.
2 Israeli na aseme sasa:
“Fadhili zake zadumu milele.”
3 Nyumba ya Haruni na iseme sasa:
“Fadhili zake zadumu milele.”
4 Wote wanaomcha Bwana na waseme sasa:
“Fadhili zake zadumu milele.”
5 Wakati wa maumivu yangu makuu, nilimlilia Bwana,
naye akanijibu kwa kuniweka huru.
6 Bwana yuko pamoja nami, sitaogopa.
Mwanadamu anaweza kunitenda nini?
7 Bwana yuko pamoja nami,
yeye ni msaidizi wangu.
Nitawatazama adui zangu
wakiwa wameshindwa.
8 Ni bora kumkimbilia Bwana
kuliko kumtumainia mwanadamu.
9 Ni bora kumkimbilia Bwana
kuliko kuwatumainia wakuu.
10 Mataifa yote yalinizunguka,
lakini kwa jina la Bwana naliwakatilia mbali.
11 Walinizunguka pande zote,
lakini kwa jina la Bwana naliwakatilia mbali.
12 Walinizunguka kama kundi la nyuki,
lakini walikufa haraka kama miiba iteketeayo;
kwa jina la Bwana naliwakatilia mbali.
13 Nilisukumwa nyuma karibu kuanguka,
lakini Bwana alinisaidia.
14 Bwana ni nguvu yangu na wimbo wangu,
yeye amefanyika wokovu wangu.
15 Sauti za shangwe na ushindi
zinavuma kwenye hema za wenye haki:
“Mkono wa kuume wa Bwana
umetenda mambo makuu!
16 Mkono wa kuume wa Bwana
umeinuliwa juu,
mkono wa kuume wa Bwana
umetenda mambo makuu!”
17 Sitakufa, bali nitaishi,
nami nitayatangaza matendo ya Bwana.
18 Bwana ameniadhibu vikali,
lakini hakuniacha nife.
19 Nifungulie malango ya haki,
nami nitaingia na kumshukuru Bwana.
20 Hili ni lango la Bwana
ambalo wenye haki wanaweza kuliingia.
21 Nitakushukuru, kwa kuwa ulinijibu,
umekuwa wokovu wangu.
22 Jiwe walilolikataa waashi,
limekuwa jiwe kuu la pembeni.
23 Bwana ametenda hili,
nalo ni la kushangaza machoni petu.
24 Hii ndiyo siku Bwana aliyoifanya,
tushangilie na kufurahi ndani yake.
25 Ee Bwana, tuokoe,
Ee Bwana, utujalie mafanikio.
26 Heri yule ajaye kwa jina la Bwana.
Kutoka nyumba ya Bwana tunakubariki.
27 Bwana ndiye Mungu,
naye ametuangazia nuru yake.
Mkiwa na matawi mkononi,
unganeni kwenye maandamano ya sikukuu
hadi kwenye pembe za madhabahu.
28 Wewe ni Mungu wangu, nitakushukuru,
wewe ni Mungu wangu, nitakutukuza.
29Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema;
fadhili zake zadumu milele.

Iliyochaguliwa sasa

Zaburi 118: NEN

Kuonyesha

Nakili

Linganisha

Shirikisha

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia