Zaburi 105
105
Zaburi 105
Uaminifu wa Mungu kwa Israeli
(1Nya 16:8‑22)
1 Mshukuruni Bwana, liitieni jina lake;
wajulisheni mataifa aliyoyatenda.
2 Mwimbieni yeye, mwimbieni yeye sifa,
waambieni matendo yake yote ya ajabu.
3 Lishangilieni jina lake takatifu,
mioyo ya wale wanaomtafuta Bwana na ifurahi.
4 Mtafuteni Bwana na nguvu zake,
utafuteni uso wake siku zote.
5 Kumbuka matendo ya ajabu aliyoyafanya,
miujiza yake na hukumu alizozitamka,
6 enyi wazao wa Abrahamu mtumishi wake,
enyi wana wa Yakobo, wateule wake.
7 Yeye ndiye Bwana Mungu wetu,
hukumu zake ziko duniani kote.
8 Hulikumbuka agano lake milele,
neno ambalo aliamuru, kwa vizazi elfu,
9 agano alilolifanya na Abrahamu,
kiapo alichomwapia Isaka.
10 Alilithibitisha kwa Yakobo kuwa amri,
kwa Israeli liwe agano la milele:
11 “Nitakupa wewe nchi ya Kanaani
kuwa sehemu utakayoirithi.”
12 Walipokuwa wachache kwa idadi,
wachache sana na wageni ndani yake,
13 walitangatanga kutoka taifa moja hadi jingine,
kutoka ufalme mmoja hadi mwingine.
14 Hakuruhusu mtu yeyote awadhulumu;
kwa ajili yao aliwakemea wafalme, akisema:
15 “Msiwaguse niliowapaka mafuta;
msiwadhuru manabii wangu.”
16 Akaiita njaa juu ya nchi
na kuharibu chakula chao chote,
17 naye akatuma mtu mbele yao,
Yusufu, aliyeuzwa kama mtumwa.
18 Walichubua miguu yake kwa minyororo,
shingo yake ilifungwa kwa chuma,
19 hadi yale aliyotangulia kusema yalipotimia,
hadi neno la Bwana lilipomthibitisha.
20 Mfalme alituma watu wakamfungua,
mtawala wa watu alimwachia huru.
21Alimfanya mkuu wa nyumba yake,
mtawala wa vyote alivyokuwa navyo,
22 kuwaelekeza wakuu wa mfalme apendavyo,
na kuwafundisha wazee wake hekima.
23 Kisha Israeli akaingia Misri,
Yakobo akaishi kama mgeni katika nchi ya Hamu.
24 Bwana aliwafanya watu wake kuzaana sana;
aliwafanya kuwa wengi sana kuliko adui zao.
25 Aliigeuza mioyo yao iwachukie watu wake,
wakatenda hila dhidi ya watumishi wake.
26 Akamtuma Musa mtumishi wake,
pamoja na Haruni, aliyemchagua.
27 Walifanya ishara zake za ajabu miongoni mwao,
miujiza yake katika nchi ya Hamu.
28 Alituma giza na nchi ikajaa giza,
kwani si walikuwa wameyaasi maneno yake?
29 Aligeuza maji yao kuwa damu,
ikasababisha samaki wao kufa.
30 Nchi yao ilijaa vyura tele, ambao waliingia
hadi kwenye vyumba vya kulala vya watawala wao.
31 Alisema, yakaja makundi ya inzi,
na viroboto katika nchi yao yote.
32 Alibadilisha mvua yao ikawa mvua ya mawe,
yenye miali ya radi nchini yao yote,
33 akaharibu mizabibu yao na miti ya tini,
na akaangamiza miti ya nchi yao.
34 Alisema, nzige wakaja,
tunutu wasio na idadi,
35wakala kila jani katika nchi yao,
wakala mazao ya ardhi yao.
36 Kisha akawaua wazaliwa wote wa kwanza katika nchi yao,
matunda ya kwanza ya ujana wao wote.
37 Akawatoa Israeli katika nchi
wakiwa na fedha na dhahabu nyingi,
wala hakuna hata mmoja
kutoka makabila yao aliyejikwaa.
38 Misri ilifurahi walipoondoka,
kwa sababu hofu ya Israeli ilikuwa imewaangukia.
39 Alitandaza wingu kama kifuniko,
na moto kuwamulikia usiku.
40 Waliomba, naye akawaletea kware,
akawashibisha kwa mkate wa mbinguni.
41 Alipasua mwamba, maji yakabubujika,
yakatiririka jangwani kama mto.
42 Kwa maana alikumbuka ahadi yake takatifu,
aliyompa Abrahamu mtumishi wake.
43 Aliwatoa watu wake kwa furaha,
wateule wake kwa kelele za shangwe,
44 akawapa nchi za mataifa, wakawa warithi wa mali
ambayo wengine walikuwa wameitaabikia:
45 alifanya haya ili wayashike mausia yake
na kuzitii sheria zake.
Msifuni Bwana.#105:45 Msifuni Bwana kwa Kiebrania ni Hallelu Yah.
Iliyochaguliwa sasa
Zaburi 105: NEN
Kuonyesha
Nakili
Linganisha
Shirikisha
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Holy Bible, Kiswahili Contemporary Version™ (Neno: Biblia Takatifu™) | Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. | Used with permission. All rights reserved worldwide.
Biblica® Cross Reference System | Copyright © 2025 by Biblica, Inc. | Used with permission. All rights reserved worldwide.