Mithali 4:14-27
Mithali 4:14-27 NENO
Usiuweke mguu wako katika njia ya waovu, wala usitembee katika njia ya wapotovu. Epukana nayo, usisafiri katika njia hiyo; achana nayo, na uelekee njia yako. Kwa kuwa hawawezi kulala hadi watende uovu; wanashindwa hata kusinzia hadi wamwangushe mtu. Wanakula mkate wa uovu, na kunywa mvinyo wa jeuri. Njia ya wenye haki ni kama nuru ya kwanza ya mapambazuko, ambayo hungʼaa zaidi na zaidi hadi mchana mkamilifu. Lakini njia ya waovu ni kama giza nene; hawajui kinachowafanya wajikwae. Mwanangu, yasikilize kwa makini yale ninayokuambia; sikiliza kwa makini maneno yangu. Usiruhusu yaondoke machoni pako, yahifadhi ndani ya moyo wako; kwa sababu ni uzima kwa wale wanaoyapata na afya kwa mwili wote wa mwanadamu. Zaidi ya yote, linda moyo wako, kuliko yote uyalindayo, maana ndiko zitokako chemchemi za uzima. Epusha kinywa chako na ukaidi; weka mazungumzo machafu mbali na midomo yako. Macho yako na yatazame mbele, kaza macho yako moja kwa moja mbele yako. Sawazisha mapito ya miguu yako na njia zako zote ziwe zimethibitika. Usigeuke kulia wala kushoto; epusha mguu wako na ubaya.