Mithali 13:10-19
Mithali 13:10-19 NENO
Kiburi huzalisha magomvi tu, bali hekima hupatikana kwa wale wanaozingatia ushauri. Fedha isiyo ya halali hupungua, bali yeye akusanyaye fedha kidogo kidogo huongezeka. Kilichotarajiwa kikikawia kuja moyo huugua, bali tumaini lililotimizwa ni mti wa uzima. Yeye anayedharau mafundisho anajiletea maangamizi, bali yeye anayeheshimu agizo hupewa tuzo. Mafundisho ya mwenye busara ni chemchemi ya uzima, ili kumwepusha mtu na mitego ya mauti. Ufahamu mzuri hupata upendeleo, bali njia ya asiye mwaminifu ni ngumu. Kila mwenye busara hutenda kwa maarifa, bali mpumbavu hudhihirisha upumbavu wake. Mjumbe mwovu huanguka kwenye taabu, bali mjumbe mwaminifu huleta uponyaji. Yeye anayedharau maonyo hupata umaskini na aibu, bali yeye anayekubali maonyo huheshimiwa. Tarajio lililotimizwa ni tamu kwa nafsi, bali wapumbavu huchukia sana kuacha ubaya.