Wafilipi 2:5-16
Wafilipi 2:5-16 NENO
Kuweni na nia ile ile aliyokuwa nayo Kristo Yesu: Yeye, ingawa alikuwa na asili ya Mungu hasa, hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa kitu cha kushikilia, bali alijifanya si kitu, akachukua hali hasa ya mtumwa, naye akazaliwa katika umbo la mwanadamu. Naye akiwa na umbo la mwanadamu, alijinyenyekeza, akatii hata mauti: naam, mauti ya msalaba! Kwa hiyo, Mungu alimtukuza juu sana, na kumpa Jina lililo kuu kuliko kila jina, ili kwa Jina la Yesu, kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi, na kila ulimi ukiri kwamba Yesu Kristo ni Bwana, kwa utukufu wa Mungu Baba. Kwa hiyo, wapendwa wangu, kama vile mmekuwa mkitii siku zote, si tu wakati nikiwa pamoja nanyi, bali sasa zaidi sana nisipokuwepo, utimizeni wokovu wenu kwa kuogopa na kutetemeka, kwa maana Mungu ndiye atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu kwa kulitimiza kusudi lake jema. Fanyeni mambo yote bila kunungʼunika wala kushindana, ili msiwe na lawama wala hatia, bali mwe wana wa Mungu wasio na kasoro katika kizazi chenye ukaidi na kilichopotoka, ambacho ndani yake ninyi mnangʼaa kama mianga ulimwenguni. Mkilishika neno la uzima, ili nipate kuona fahari siku ya Kristo kwamba sikupiga mbio wala kujitaabisha bure.