Wafilipi 2:1-11
Wafilipi 2:1-11 NENO
Kama kukiwa na jambo lolote la kutia moyo katika kuunganishwa na Al-Masihi, kukiwa faraja yoyote katika upendo wake, kukiwa na ushirika wowote na Roho wa Mungu, kukiwa na wema wowote na huruma, basi ikamilisheni furaha yangu kwa kuwa na nia moja, mkiwa na upendo huo moja, mkiwa wa roho na kusudi moja. Msitende jambo lolote kwa nia ya kujitukuza wala kujivuna, bali kwa unyenyekevu kila mtu amhesabu mwingine bora kuliko nafsi yake. Kila mmoja wenu asiangalie faida yake mwenyewe tu, bali pia ajishughulishe kwa faida ya wengine. Kuweni na nia ile ile aliyokuwa nayo Al-Masihi Isa: Yeye, ingawa alikuwa na asili ya Mungu hasa, hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa kitu cha kushikilia, bali alijifanya si kitu, akachukua hali hasa ya mtumwa, naye akazaliwa katika umbo la mwanadamu. Naye akiwa na umbo la mwanadamu, alijinyenyekeza, akatii hata mauti: naam, mauti ya msalaba! Kwa hiyo, Mungu alimtukuza juu sana, na kumpa Jina lililo kuu kuliko kila jina, ili kwa Jina la Isa, kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi, na kila ulimi ukiri kwamba Isa Al-Masihi ni Bwana, kwa utukufu wa Mungu Baba Mwenyezi.