Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Marko 4:1-20

Marko 4:1-20 NENO

Yesu akaanza kufundisha tena kando ya bahari. Palikuwa na umati mkubwa wa watu waliokuwa wamekusanyika kumzunguka, hata ikambidi Yesu aingie kwenye mashua iliyokuwa baharini na kuketi humo, nao watu wote walikuwa ufuoni mwa bahari. Akawafundisha mambo mengi kwa mifano, naye katika mafundisho yake akasema: “Sikilizeni! Tazama, mpanzi alitoka kwenda kupanda mbegu Alipokuwa akitawanya mbegu, nyingine zilianguka kando ya njia, nao ndege wakaja na kuzila. Nyingine zilianguka kwenye mwamba usio na udongo mwingi. Ziliota haraka kwa kuwa udongo ulikuwa kidogo. Lakini jua lilipozidi, mimea ikanyauka na kukauka kwa kuwa mizizi yake haikuwa na kina. Mbegu nyingine zilianguka kwenye miiba, nayo miiba ikakua, ikaisonga hiyo mimea, hivyo haikutoa mazao. Mbegu nyingine zilianguka kwenye udongo mzuri, zikaota vizuri na kukua, zikatoa mazao, moja mara thelathini, nyingine mara sitini, na nyingine mara mia moja.” Kisha Yesu akasema, “Mwenye masikio ya kusikia, na asikie.” Alipokuwa peke yake, watu waliokuwa naye pamoja na wanafunzi wake kumi na wawili wakamuuliza kuhusu mifano yake. Naye akawaambia, “Ninyi mmepewa siri ya ufalme wa Mungu. Lakini kwa wale walio nje, kila kitu husemwa kwa mifano, ili, “ ‘kuona waone lakini wasitambue, na kusikia wasikie lakini wasielewe; wasije wakageuka na kusamehewa!’” Kisha Yesu akawauliza, “Hamwelewi maana ya mfano huu? Basi mtaelewaje mifano mingine? Yule mpanzi hupanda neno. Hawa ndio wale walio kando ya njia ambako neno lilipandwa. Walisikiapo neno, mara Shetani huja na kulinyakua lile neno lililopandwa ndani yao. Nazo zile mbegu zilizoanguka kwenye udongo wenye miamba, ni wale wanaolisikia neno, na mara hulipokea kwa furaha. Lakini kwa kuwa hawana mizizi, wao hudumu kwa muda mfupi tu. Kisha dhiki au mateso yanapoinuka kwa ajili ya lile neno, mara wao huiacha imani. Lakini wengine, kama mbegu iliyopandwa kwenye miiba, hulisikia lile neno; lakini masumbufu ya maisha haya, na udanganyifu wa mali na tamaa ya mambo mengine huja na kulisonga lile neno na kulifanya lisizae. Wengine, kama mbegu iliyopandwa kwenye udongo mzuri, hulisikia lile neno, wakalipokea na kuzaa mazao. Wao huzaa mara thelathini, au mara sitini, au mara mia ya mbegu iliyopandwa.”

Video zinazohusiana