Mathayo 27:11-23
Mathayo 27:11-23 NENO
Wakati huo Yesu akiwa amesimama mbele ya mtawala, mtawala akamuuliza, “Wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi?” Yesu akasema, “Wewe wasema hivyo.” Lakini viongozi wa makuhani na wazee walipomshtaki, hakujibu neno. Ndipo Pilato akamuuliza, “Je, husikii ni mambo mangapi wanayokushtaki nayo?” Lakini Yesu hakumjibu hata kwa shtaka moja, kiasi kwamba mtawala alishangaa sana. Basi ilikuwa ni desturi ya mtawala kumfungua mfungwa mmoja aliyechaguliwa na umati wa watu wakati wa sikukuu. Palikuwa na mfungwa mmoja mwenye sifa mbaya, aliyeitwa Baraba. Hivyo umati wa watu walipokusanyika, Pilato akawauliza hao watu, “Mnataka niwafungulie yupi: Baraba au Yesu aitwaye Kristo?” Kwa kuwa alitambua kwamba walikuwa wamemkabidhi Yesu kwake kwa ajili ya wivu. Pilato akiwa ameketi kwenye kiti cha hukumu, mkewe akampelekea ujumbe huu: “Usiwe na jambo lolote juu ya mtu huyu asiye na hatia, kwa kuwa leo nimeteseka sana katika ndoto kwa sababu yake.” Lakini viongozi wa makuhani na wazee wakashawishi umati wa watu kwamba waombe Baraba afunguliwe, naye Yesu auawe. Mtawala akawauliza tena, “Ni yupi kati ya hawa wawili mnayetaka niwafungulie?” Wakajibu, “Baraba.” Pilato akawaambia, “Basi nifanye nini na huyu Yesu aitwaye Kristo?” Wakajibu wote, “Msulubishe!” Pilato akauliza, “Kwa nini? Amefanya kosa gani?” Lakini wao wakazidi kupiga kelele, wakisema, “Msulubishe!”




