Mathayo 24:1-22
Mathayo 24:1-22 NENO
Yesu akatoka Hekaluni na alipokuwa akienda zake, wanafunzi wake wakamwendea ili kumwonesha majengo ya Hekalu. Ndipo Yesu akawauliza, “Je, mnayaona haya yote? Amin, nawaambia, hakuna hata jiwe moja hapa litakalobaki juu ya jingine, bali kila moja litabomolewa.” Yesu alipokuwa ameketi kwenye Mlima wa Mizeituni, wanafunzi wake wakamjia faraghani, wakamuuliza, “Tuambie, mambo haya yatatukia lini, nayo dalili ya kuja kwako na ya mwisho wa dunia ni gani?” Yesu akawajibu, “Jihadharini, mtu yeyote asiwadanganye. Kwa maana wengi watakuja kwa Jina langu, wakidai, ‘Mimi ndiye Kristo,’ nao watawadanganya wengi. Mtasikia habari za vita na tetesi za vita. Angalieni msitishike, kwa maana haya hayana budi kutukia. Lakini ule mwisho bado. Taifa litainuka dhidi ya taifa, na ufalme dhidi ya ufalme. Kutakuwa na njaa na mitetemeko ya ardhi sehemu mbalimbali. Haya yote yatakuwa ndio mwanzo wa uchungu. “Ndipo mtasalitiwa, ili mteswe na kuuawa, nanyi mtachukiwa na mataifa yote kwa ajili yangu. Wakati huo, wengi wataacha imani yao, nao watasalitiana kila mmoja na mwenzake na kuchukiana. Watatokea manabii wengi wa uongo, nao watawadanganya watu wengi. Kwa sababu ya kuongezeka kwa uovu, upendo wa watu wengi utapoa, lakini yule atakayevumilia hadi mwisho ataokolewa. Injili hii ya ufalme itahubiriwa ulimwenguni kote kuwa ushuhuda kwa mataifa yote. Ndipo mwisho utakapokuja. “Hivyo mtakapoona lile ‘chukizo la uharibifu’ lililonenwa na nabii Danieli limesimama mahali patakatifu (asomaye na afahamu), basi wale walio Yudea wakimbilie milimani. Yeyote aliye juu ya dari ya nyumba asishuke ili kuchukua chochote kutoka ndani ya nyumba. Aliye shambani asirudi nyumbani kuchukua vazi lake. Ole wao wenye mimba na wale wanaonyonyesha watoto siku hizo! Ombeni ili kukimbia kwenu kusiwe wakati wa baridi au siku ya Sabato. Kwa maana wakati huo kutakuwa na dhiki kuu ambayo haijapata kuwepo tangu mwanzo wa dunia hadi sasa: wala haitakuwepo tena kamwe. “Kama siku hizo zisingefupishwa, hakuna mtu ambaye angeokoka. Lakini kwa ajili ya wateule, siku hizo zitafupishwa.