Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mathayo 20:20-34

Mathayo 20:20-34 NENO

Kisha mama yao wana wa Zebedayo akamjia Yesu pamoja na wanawe, naye akapiga magoti mbele yake, akamwomba Yesu amfanyie jambo fulani. Yesu akamuuliza, “Unataka nini?” Akajibu, “Tafadhali, wajalie wanangu hawa ili mmoja aketi upande wako wa kuume, na mwingine upande wako wa kushoto katika ufalme wako.” Yesu akawaambia, “Ninyi hamjui mnaloliomba. Je, mnaweza kukinywea kikombe nitakachonywea mimi?” Wakajibu, “Tunaweza.” Yesu akawaambia, “Kwa kweli kikombe changu mtakinywea, lakini kuketi upande wangu wa kuume au wa kushoto si langu mimi kuwapa. Nafasi hizo ni za wale ambao wameandaliwa na Baba yangu.” Wale wanafunzi wengine kumi waliposikia haya, waliwakasirikia hao ndugu wawili. Lakini Yesu akawaita wote pamoja na kuwaambia, “Mnafahamu kuwa watawala wa watu wa Mataifa huwatawala kwa nguvu, nao wenye vyeo huonesha mamlaka yao. Isiwe hivyo kwenu. Badala yake, yeyote anayetaka kuwa mkuu miongoni mwenu hana budi kuwa mtumishi wenu, naye anayetaka kuwa wa kwanza miongoni mwenu hana budi kuwa mtumwa wenu: kama vile Mwana wa Adamu hakuja kutumikiwa, bali kutumika na kuutoa uhai wake uwe fidia kwa ajili ya wengi.” Yesu na wanafunzi wake walipokuwa wakiondoka Yeriko, umati mkubwa wa watu wakamfuata. Vipofu wawili walikuwa wameketi kando ya barabara. Waliposikia kwamba Yesu alikuwa anapita, wakapaza sauti wakisema, “Bwana, Mwana wa Daudi, tuhurumie!” Umati wa watu wakawakemea na kuwaambia wanyamaze, lakini wao wakazidi kupaza sauti wakisema, “Bwana, Mwana wa Daudi, tuhurumie.” Yesu akasimama na kuwaita, akawauliza, “Mnataka niwafanyie nini?” Wakamjibu, “Bwana, tunataka kuona.” Yesu akawahurumia na kuwagusa macho yao. Mara macho yao yakapata kuona, nao wakamfuata.