Mathayo 2:1-18
Mathayo 2:1-18 NENO
Baada ya Yesu kuzaliwa katika mji wa Bethlehemu huko Yudea, wakati wa utawala wa Mfalme Herode, wataalamu wa mambo ya nyota kutoka mashariki walifika Yerusalemu wakiuliza, “Yuko wapi huyo aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tumeona nyota yake ikitokea mashariki, nasi tumekuja kumwabudu.” Mfalme Herode aliposikia jambo hili aliingiwa na hofu sana pamoja na watu wote wa Yerusalemu. Herode akawaita pamoja viongozi wa makuhani na walimu wa sheria, akawauliza ni wapi ambapo Kristo angezaliwa. Nao wakamwambia, “Katika Bethlehemu ya Yudea, kwa maana hivyo ndivyo ilivyoandikwa na nabii: “ ‘Nawe, Bethlehemu, katika nchi ya Yuda, wewe si mdogo miongoni mwa watawala wa Yuda; kwa maana kutoka kwako atakuja mtawala atakayekuwa mchungaji wa watu wangu Israeli.’” Ndipo Herode akawaita wale wataalamu wa nyota kwa siri na kutaka kujua kutoka kwao uhakika kamili wa wakati ile nyota ilionekana. Kisha akawatuma Bethlehemu na kuwaambia, “Nendeni mkamtafute mtoto huyo kwa makini. Mara tu mtakapompata, nileteeni taarifa ili nami niende kumwabudu.” Baada ya kumsikia mfalme, wale wataalamu wa nyota wakaenda zao, nayo ile nyota waliyoiona mashariki ikawatangulia, nao wakaifuata hadi iliposimama mahali alipokuwa mtoto. Walipoiona ile nyota wakajawa na furaha kubwa mno. Walipoingia ndani ya ile nyumba, wakamwona mtoto pamoja na Mariamu mama yake, wakamsujudia na kumwabudu yule mtoto Yesu. Ndipo wakafungua hazina zao, wakamtolea zawadi za dhahabu, uvumba na manemane. Kwa kuwa walikuwa wameonywa katika ndoto wasirudi kwa Herode, wakarudi nchi yao kwa njia nyingine. Walipokwisha kwenda zao, malaika wa Bwana akamtokea Yusufu katika ndoto akamwambia, “Amka, umchukue mtoto na mama yake, mkimbilie Misri. Kaeni huko hadi nitakapowaambia, kwa maana Herode anataka kumtafuta huyu mtoto ili amuue.” Kisha Yusufu akaamka, akamchukua mtoto pamoja na mama yake wakati wa usiku, nao wakaenda Misri, ambako walikaa hadi Herode alipofariki. Hili lilifanyika ili litimie lile neno Bwana alilosema kupitia kwa nabii: “Nilimwita mwanangu kutoka Misri.” Herode alipogundua kwamba alikuwa amedanganywa na wale wataalamu wa nyota, alikasirika sana, naye akatoa amri ya kuwaua watoto wote wa kiume wenye umri wa miaka miwili kurudi chini katika mji wa Bethlehemu na sehemu zote za jirani, kwa mujibu wa ule muda alioambiwa na wale wataalamu wa nyota. Ndipo lilipotimia neno lililonenwa na nabii Yeremia, aliposema: “Sauti ilisikika huko Rama, maombolezo na kilio kikubwa, Raheli akilia kwa ajili ya wanawe, akikataa kufarijiwa, kwa sababu hawako tena.”