Mathayo 18:15-22
Mathayo 18:15-22 NENO
“Ndugu yako akikukosea, nenda ukamwoneshe kosa lake, kati yenu ninyi wawili peke yenu. Akikusikiliza, utakuwa umempata tena ndugu yako. Lakini asipokusikiliza, nenda na mtu mwingine mmoja au wawili ili kila neno ‘lithibitishwe kwa ushahidi wa mashahidi wawili au watatu’. Akikataa kuwasikiliza hao, liambie kanisa. Naye akikataa hata kulisikiliza kanisa, basi awe kwenu kama mtu asiyeamini au mtoza ushuru. “Amin, nawaambia, lolote mtakalolifunga duniani litakuwa limefungwa mbinguni, na lolote mtakalolifungua duniani litakuwa limefunguliwa mbinguni. “Tena nawaambia, ikiwa wawili wenu watakubaliana duniani kuhusu jambo lolote watakaloomba, watatendewa na Baba yangu aliye mbinguni. Kwa kuwa wanapokusanyika pamoja watu wawili au watatu kwa Jina langu, mimi niko papo hapo pamoja nao.” Kisha Petro akamwendea Yesu na kumuuliza, “Bwana, ni mara ngapi nimsamehe ndugu yangu akinikosea? Hadi mara saba?” Yesu akamjibu, “Sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini.