Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mathayo 17:1-9

Mathayo 17:1-9 NENO

Siku sita baada ya jambo hili, Yesu akawachukua Petro, Yakobo na Yohana ndugu yake Yakobo, akawapeleka juu ya mlima mrefu peke yao. Wakiwa huko, Yesu alibadilika sura mbele yao. Uso wake ukangʼaa kama jua na nguo zake zikawa nyeupe kama nuru. Ghafula wakawatokea mbele yao Musa na Eliya, wakizungumza na Yesu. Ndipo Petro akamwambia Yesu, “Bwana, ni vyema sisi tukae hapa. Ukitaka, nitafanya vibanda vitatu: kimoja chako, kingine cha Musa na kingine cha Eliya.” Petro alipokuwa angali ananena, ghafula wingu lililongʼaa likawafunika, na sauti ikatoka kwenye hilo wingu ikisema, “Huyu ni Mwanangu mpendwa. Ninapendezwa naye sana. Msikieni yeye.” Wanafunzi waliposikia haya, wakaanguka kifudifudi, wakajawa na hofu. Lakini Yesu akaja na kuwagusa, akawaambia, “Inukeni na wala msiogope.” Walipoinua macho yao, hawakumwona mtu mwingine yeyote isipokuwa Yesu. Walipokuwa wakishuka kutoka mlimani, Yesu akawaagiza, “Msimwambie mtu yeyote mambo mliyoyaona hapa, hadi Mwana wa Adamu atakapofufuliwa kutoka kwa wafu.”