Mathayo 14:13-22
Mathayo 14:13-22 NENO
Yesu aliposikia yaliyokuwa yametukia, aliondoka kwa chombo akaenda mahali pasipo na watu ili awe peke yake. Lakini watu walipopata habari, wakamfuata kwa miguu kupitia nchi kavu kutoka miji. Yesu alipofika kando ya bahari, aliona makundi makubwa ya watu, akawahurumia na akawaponya wagonjwa wao. Ilipofika jioni, wanafunzi wake walienda kwake, wakamwambia, “Mahali hapa ni nyikani, na muda sasa umekwisha. Waage makundi ya watu ili waende zao vijijini wakajinunulie chakula.” Yesu akawaambia, “Hakuna sababu ya wao kuondoka. Ninyi wapeni chakula.” Wakamjibu, “Tuna mikate mitano na samaki wawili tu.” Akawaambia, “Nileteeni hivyo vitu hapa.” Yesu akaagiza umati wa watu wakae chini kwenye nyasi. Akaichukua ile mikate mitano na wale samaki wawili, akainua macho yake akatazama mbinguni, akavibariki na kuimega ile mikate. Kisha akawapa wanafunzi, nao wanafunzi wakawagawia ule umati. Wote wakala, wakashiba. Nao wanafunzi wakakusanya vipande vilivyosalia, wakajaza vikapu kumi na viwili. Idadi ya watu waliokula walikuwa wanaume wapatao elfu tano, bila kuhesabu wanawake na watoto. Mara Yesu akawaambia wanafunzi wake waingie katika mashua wamtangulie kwenda ngʼambo ya bahari, wakati yeye alikuwa akiaga ule umati.