Maombolezo 1:1-11
Maombolezo 1:1-11 NENO
Tazama jinsi mji ulivyoachwa ukiwa, mji ambao zamani ulikuwa umejaa watu! Jinsi umekuwa kama mama mjane, ambaye wakati fulani alikuwa maarufu miongoni mwa mataifa! Yule aliyekuwa malkia miongoni mwa majimbo sasa amekuwa mtumwa. Kwa uchungu, hulia sana usiku, machozi yapo kwenye mashavu yake. Miongoni mwa wapenzi wake wote hakuna yeyote wa kumfariji. Rafiki zake wote wamemsaliti, wamekuwa adui zake. Baada ya mateso na kufanyishwa kazi kikatili, Yuda ameenda uhamishoni. Anakaa miongoni mwa mataifa, hapati mahali pa kupumzika. Wote ambao wanamsaka wamemkamata katikati ya dhiki yake. Barabara zielekeazo Sayuni zaomboleza, kwa kuwa hakuna yeyote anayekuja kwenye sikukuu zake zilizoamriwa. Malango yake yote yamekuwa ukiwa, makuhani wake wanalia kwa uchungu, wanawali wake wanahuzunika, naye yuko katika uchungu wa maumivu makuu. Adui zake wamekuwa mabwana zake, watesi wake wana amani. BWANA amemletea huzuni kwa sababu ya dhambi zake nyingi. Watoto wake wameenda uhamishoni, wamekuwa mateka mbele ya adui. Fahari zilizokuwa zake zimeondoka kutoka kwa Binti Sayuni. Wakuu wake wako kama ayala ambaye hapati malisho, wakiwa dhaifu wamekimbia mbele ya aliyewakimbiza. Katika siku za mateso yake na kutangatanga, Yerusalemu hukumbuka hazina zote ambazo zilikuwa zake siku za kale. Watu wake walipoanguka katika mikono ya adui, hapatakuwa na yeyote wa kumsaidia. Watesi wake walimtazama na kumcheka katika maangamizi yake. Yerusalemu ametenda dhambi sana kwa hiyo amekuwa najisi. Wote waliomheshimu wanamdharau, kwa maana wameuona uchi wake. Yeye mwenyewe anapiga kite na kugeukia mbali. Uchafu wake umegandamana na nguo zake; hakuwaza juu ya maisha yake ya baadaye. Anguko lake lilikuwa la kushangaza, hapakuwa na yeyote wa kumfariji. “Tazama, Ee BWANA, teso langu, kwa maana adui ameshinda.” Adui ametia mikono juu ya hazina zake zote, aliona mataifa ya kipagani wakiingia mahali patakatifu pake, wale uliowakataza kuingia kwenye kusanyiko lako. Watu wake wote wanalia kwa uchungu watafutapo chakula; wanabadilisha hazina zao kwa chakula ili waweze kuendelea kuishi. “Tazama, Ee BWANA, uangalie; kwa maana nimedharauliwa.”


