Ayubu 34:1-15
Ayubu 34:1-15 NENO
Kisha Elihu akasema: “Sikieni maneno yangu, enyi watu wenye hekima; nisikilizeni mimi, ninyi watu wenye maarifa. Kwa kuwa sikio huyajaribu maneno kama vile ulimi uonjavyo chakula. Tujichagulie wenyewe yaliyo sawa, nasi tujifunze pamoja yaliyo mema. “Ayubu anasema, ‘Mimi sina hatia, lakini Mungu ameninyima haki yangu. Ingawa niko sawa, ninaonekana mwongo; nami ingawa sina kosa, kidonda changu hakiponi.’ Ni mtu gani aliye kama Ayubu, anywaye dharau kama maji? Hushirikiana na watenda maovu, na kuchangamana na watu waovu. Kwa kuwa anasema, ‘Haimfaidi mwanadamu kitu chochote anapojitahidi kumpendeza Mungu.’ “Hivyo nisikilizeni mimi, ninyi watu wenye ufahamu. Kamwe Mungu hatendi uovu, Mwenyezi hafanyi kosa. Humlipa mwanadamu kwa ajili ya lile alilotenda; huleta juu yake kile ambacho matendo yake yanastahili. Ni jambo lisilofikirika kwamba Mungu angefanya makosa, kwamba Mwenyezi angepotosha hukumu. Je, ni nani aliyemtawaza juu ya dunia? Ni nani aliyemweka kuwa mwangalizi wa ulimwengu wote? Kama lilikuwa kusudi la Mungu, naye akaiondoa Roho yake na pumzi yake, wanadamu wote wangeangamia kwa pamoja, na mtu angerudi mavumbini.