Ayubu 1:6-22
Ayubu 1:6-22 NENO
Siku moja wana wa Mungu walienda kujionesha mbele za BWANA. Shetani naye akaja pamoja nao. BWANA akamwambia Shetani, “Umetoka wapi?” Shetani akamjibu BWANA, “Natoka kuzunguka duniani, nikitembea huku na huko.” Ndipo BWANA akamwambia Shetani, “Je, umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Hakuna mtu mwingine duniani aliye kama yeye, asiye na hatia, ni mnyofu, mwenye kumcha Mungu, na kuepukana na uovu.” Shetani akamjibu BWANA, “Je, Ayubu anamcha Mungu bure? Je, wewe hukumzingira pande zote, yeye na watu wa nyumbani mwake, pamoja na kila kitu alicho nacho? Kazi za mikono yake umezibariki, na hivyo makundi yake ya kondoo na mbuzi pamoja na ya wanyama yameenea katika nchi nzima. Lakini nyoosha mkono wako na kupiga kila kitu alicho nacho, naye kwa hakika atakulaani mbele za uso wako.” BWANA akamwambia Shetani, “Vema sana, kwa hiyo, kila kitu alicho nacho kiko mikononi mwako, lakini huyo mtu mwenyewe usimguse hata kwa kidole.” Ndipo Shetani akatoka mbele za BWANA. Siku moja watoto wa Ayubu walipokuwa wakifanya karamu wakila na kunywa divai katika nyumba ya ndugu yao mkubwa, akaja mjumbe kwa Ayubu na kusema, “Maksai walikuwa wakilima na punda walikuwa wakilisha karibu nao, Waseba wakawashambulia na kuchukua mifugo. Kisha wakawaua watumishi kwa upanga, mimi peke yangu ndiye niliyenusurika kukuletea habari!” Alipokuwa bado ananena, mjumbe mwingine akaja na kusema, “Moto wa Mungu ulishuka kutoka mbinguni na kuteketeza kondoo na watumishi, mimi peke yangu ndiye niliyenusurika kukuletea habari!” Alipokuwa bado ananena, mjumbe mwingine akaja na kusema, “Wakaldayo waliunda vikosi vitatu vya uvamizi na kuwaangukia ngamia wako na kuwachukua wakaondoka nao. Wakawaua watumishi kwa upanga, mimi peke yangu ndiye niliyenusurika kukuletea habari.” Alipokuwa bado ananena, mjumbe mwingine akaja na kusema, “Wana wako wa kiume na wa kike walipokuwa wakifanya karamu, wakila na kunywa divai katika nyumba ya ndugu yao mkubwa, ghafula upepo wenye nguvu ukavuma kutoka jangwani, nao ukaipiga nyumba hiyo pembe zake nne. Ikawaangukia hao watoto nao wamekufa, mimi peke yangu ndiye niliyenusurika kukuletea habari!” Ndipo Ayubu akasimama, akararua joho lake na kunyoa nywele zake. Kisha akasujudu na kuabudu, akasema: “Nilitoka tumboni mwa mama yangu uchi, nami nitaondoka uchi, BWANA alinipa, naye BWANA ameviondoa; jina la BWANA litukuzwe.” Katika mambo haya yote, Ayubu hakutenda dhambi kwa kumlaumu Mungu kwa kufanya ubaya.


