Yohana 4:7-15
Yohana 4:7-15 NENO
Mwanamke mmoja Msamaria alipokuja kuteka maji, Yesu akamwambia, “Naomba maji ninywe.” (Wakati huo wanafunzi wake walikuwa wameenda mjini kununua chakula.) Yule mwanamke Msamaria akamjibu, “Wewe ni Myahudi na mimi ni Msamaria. Yawezekanaje uniombe maji ya kunywa?” (Wayahudi walikuwa hawashirikiani kabisa na Wasamaria.) Yesu akamjibu, “Kama ungeijua karama ya Mungu, na ni nani anakuomba maji ya kunywa, ungemwomba yeye, naye angekupa maji ya uzima.” Yule mwanamke akamjibu, “Bwana, wewe huna chombo cha kutekea maji na kisima hiki ni kirefu. Hayo maji ya uzima utayapata wapi? Kwani wewe ni mkuu kuliko baba yetu Yakobo ambaye alitupatia kisima hiki, ambacho yeye pamoja na watoto wake na mifugo yake walikitumia?” Yesu akamjibu, “Kila mtu anayekunywa maji ya kisima hiki ataona kiu tena. Lakini yeyote anywaye maji nitakayompa hataona kiu kamwe. Maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji, yakibubujika uzima wa milele.” Yule mwanamke akamwambia, “Bwana, tafadhali nipe maji hayo ili nisipate kiu tena, wala nisije tena hapa kuteka maji!”