Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yohana 20:11-18

Yohana 20:11-18 NENO

Lakini Mariamu Magdalene akasimama nje ya kaburi akilia. Alipokuwa akilia, akainama kuchungulia mle kaburini, naye akaona malaika wawili wamevaa mavazi meupe, wameketi pale mwili wa Yesu ulipokuwa umelazwa, mmoja upande wa kichwani na mwingine upande wa miguuni. Wakamuuliza Mariamu, “Mwanamke, mbona unalia?” Akawaambia, “Nalia kwa kuwa wamemchukua Bwana wangu, na sijui walikomweka.” Baada ya kusema hayo, akageuka, akamwona Yesu amesimama, lakini hakumtambua. Yesu akamwambia, “Mwanamke, mbona unalia? Unamtafuta nani?” Mariamu, akidhani alikuwa anaongea na mtunza bustani, akamwambia, “Bwana, kama ni wewe umemchukua, tafadhali nioneshe ulikomweka, nami nitamchukua.” Yesu akamwita, “Mariamu!” Ndipo Mariamu akamgeukia Yesu na kusema naye kwa Kiebrania, “Raboni!” (maana yake “Mwalimu”). Yesu akamwambia, “Usinishike, kwa maana sijapaa kwenda kwa Baba. Lakini nenda kwa ndugu zangu ukawaambie, ‘Ninapaa kwenda kwa Baba yangu ambaye ni Baba yenu, kwa Mungu wangu ambaye ni Mungu wenu.’ ” Kwa hiyo Mariamu Magdalene akaenda kuwatangazia wanafunzi wa Yesu, akisema, “Nimemwona Bwana!” Naye akawaambia kwamba Yesu alikuwa amemweleza mambo hayo yote.