Yohana 20:1-10
Yohana 20:1-10 NENO
Alfajiri na mapema siku ya kwanza ya juma, kulipokuwa bado giza, Mariamu Magdalene alienda kaburini na kukuta lile jiwe limeondolewa penye ingilio. Hivyo akakimbia kwa Simoni Petro pamoja na yule mwanafunzi mwingine ambaye Yesu alimpenda, na kusema, “Wamemwondoa Bwana kaburini, na hatujui walikomweka!” Petro na yule mwanafunzi mwingine wakaondoka mara moja kuelekea kaburini. Wote wawili walikuwa wanakimbia, lakini yule mwanafunzi mwingine akakimbia mbio kuliko Petro, akatangulia kufika kaburini. Akainama na kuchungulia mle kaburini, akaona vile vitambaa vya kitani, lakini hakuingia. Ndipo Simoni Petro akaja akimfuata nyuma, akaingia ndani ya kaburi. Naye akaona vile vitambaa vya ile sanda vikiwa pale chini, na kile kitambaa kilichokuwa kichwani mwa Yesu. Kitambaa hicho kilikuwa kimekunjwa peke yake, mbali na vile vitambaa vya kitani vya ile sanda. Kisha yule mwanafunzi aliyetangulia kufika kaburini akaingia ndani, akaona, na akaamini. (Kwa kuwa hadi wakati huo walikuwa bado hawajaelewa kutoka Maandiko kwamba ilikuwa lazima Yesu afufuke kutoka kwa wafu.) Kisha hao wanafunzi wakaondoka, wakarudi nyumbani mwao.