Yohana 12:1-19
Yohana 12:1-19 NENO
Siku sita kabla ya Pasaka, Yesu alienda Bethania, makao ya Lazaro, aliyekuwa amemfufua kutoka kwa wafu. Wakaandaa karamu kwa heshima ya Yesu. Martha akawahudumia, wakati Lazaro alikuwa miongoni mwa waliokaa mezani pamoja na Yesu. Kisha Mariamu akachukua chupa ya painti moja yenye manukato ya nardo safi ya thamani kubwa, akayamimina miguuni mwa Yesu na kuifuta kwa nywele zake. Nyumba nzima ikajaa harufu nzuri ya manukato. Ndipo Yuda Iskariote mwana wa Simoni, mmoja wa wanafunzi wa Yesu, ambaye baadaye angemsaliti Yesu, akasema, “Kwa nini manukato haya hayakuuzwa kwa dinari mia tatu, na fedha hizo wakapewa maskini?” Yuda hakusema hivi kwa kuwa aliwajali maskini, bali kwa kuwa alikuwa mwizi; ndiye alikuwa akitunza mfuko wa fedha, na akawa akiiba zile fedha. Yesu akasema, “Mwacheni. Aliyanunua manukato hayo ili ayaweke kwa ajili ya siku ya maziko yangu. Maskini mtakuwa nao siku zote, lakini mimi hamtakuwa nami siku zote.” Umati mkubwa wa Wayahudi walipojua kwamba Yesu alikuwa huko Bethania, walikuja si tu kwa ajili ya Yesu, lakini pia kumwona Lazaro ambaye Yesu alikuwa amemfufua. Kwa hiyo viongozi wa makuhani wakapanga njama ya kumuua Lazaro pia, kwa kuwa kutokana na habari za kufufuliwa kwake, Wayahudi wengi walikuwa wanamfuata Yesu na kumwamini. Siku iliyofuata umati mkubwa wa watu waliokuwa wamekuja kwenye Sikukuu walisikia kwamba Yesu angekuja Yerusalemu. Basi wakachukua matawi ya mitende, wakatoka kwenda kumlaki, huku wakipaza sauti wakisema, “Hosana!” “Amebarikiwa yeye ajaye kwa Jina la Bwana!” “Amebarikiwa mfalme wa Israeli!” Yesu akamkuta mwana-punda, akampanda, kama ilivyoandikwa, “Usiogope, ewe Binti Sayuni; tazama, mfalme wako anakuja, amepanda mwana-punda!” Wanafunzi wake Yesu mwanzoni hawakuelewa mambo haya. Lakini Yesu alipotukuzwa, ndipo walipokumbuka kuwa mambo haya yalikuwa yameandikwa kwa ajili yake na alitendewa yeye. Wale waliokuwepo Yesu alipomwita Lazaro kutoka kaburini na kumfufua kutoka kwa wafu waliendelea kushuhudia. Na kwa sababu walikuwa wamesikia kwamba alikuwa ametenda muujiza huu, umati wa watu wakaenda kumlaki. Hivyo Mafarisayo walipoona hayo, wakaambiana, “Mnaona, hamwezi kufanya lolote. Angalieni, ulimwengu wote unamfuata yeye!”