Yeremia 29:1-23
Yeremia 29:1-23 NENO
Haya ndio maneno ya barua ambayo nabii Yeremia aliituma kutoka Yerusalemu kwenda kwa wazee waliobaki miongoni mwa waliopelekwa uhamishoni, na kwa makuhani, manabii na watu wengine wote ambao Nebukadneza alikuwa amewachukua kwenda uhamishoni Babeli kutoka Yerusalemu. (Hii ilikuwa ni baada ya Mfalme Yekonia na mama malkia, maafisa wa mahakama, viongozi wa Yuda na wa Yerusalemu, mafundi na wahunzi kwenda uhamishoni kutoka Yerusalemu.) Barua ilikabidhiwa kwa Elasa mwana wa Shafani, na kwa Gemaria mwana wa Hilkia, ambao Sedekia mfalme wa Yuda aliwatuma kwa Mfalme Nebukadneza huko Babeli. Barua yenyewe ilisema: Hili ndilo BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, awaambialo wale wote niliowapeleka kutoka Yerusalemu kwenda uhamishoni Babeli: “Jengeni nyumba na mwishi humo, pandeni bustani na mle mazao yake. Oeni wake na mzae watoto wa kiume na wa kike; watafutieni wake watoto wenu wa kiume, na waozeni binti zenu ili nao wazae watoto wa kiume na wa kike; mkaongezeke huko, wala msipungue idadi. Pia tafuteni amani na mafanikio ya mji ambamo nimewapeleka uhamishoni. Mwombeni BWANA kwa ajili ya mji huo, kwa sababu ukistawi, ninyi pia mtastawi.” Naam, hili ndilo BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, asemalo: “Msikubali manabii na waaguzi walio miongoni mwenu wawadanganye. Msisikilize ndoto ambazo mmewatia moyo kuota. Wanawatabiria ninyi uongo kwa jina langu. Sikuwatuma,” asema BWANA. Hili ndilo asemalo BWANA: “Miaka sabini itakapotimia kwa ajili ya Babeli, nitakuja kwenu na kutimiza ahadi yangu ya rehema ya kuwarudisha mahali hapa. Kwa maana ninajua mipango niliyo nayo kwa ajili yenu,” asema BWANA, “ni mipango ya kuwafanikisha na wala si ya kuwadhuru, ni mipango ya kuwapa tumaini katika siku zijazo. Kisha mtaniita, na mtakuja na kuniomba, nami nitawasikiliza. Mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wote. Nitaonekana kwenu,” asema BWANA, “nami nitawarudisha watu wenu waliotekwa. Nitawakusanya kutoka mataifa yote na mahali pote nilipokuwa nimewafukuzia, nami nitawarudisha mahali nilipokuwa nimewatoa walipopelekwa uhamishoni,” asema BWANA. Mnaweza mkasema, “BWANA ameinua manabii kwa ajili yetu huku Babeli,” lakini hili ndilo asemalo BWANA kuhusu mfalme aketiye katika kiti cha utawala cha Daudi, na watu wa kwenu wote wanaobaki katika mji huu, ndugu zenu ambao hawakuenda pamoja nanyi uhamishoni. Naam, hili ndilo asemalo BWANA wa majeshi: “Nitatuma upanga, njaa na tauni dhidi yao, nami nitawafanya kuwa kama tini mbovu zilizooza, zisizofaa kuliwa. Nitawafukuza kwa upanga, kwa njaa na kwa tauni, nami nitawafanya kuwa chukizo kwa falme zote za dunia, kitu cha laana na cha kutisha, kisichofaa na cha kuzomewa miongoni mwa mataifa nitakakowafukuzia. Kwa kuwa hawakuyasikiliza maneno yangu,” asema BWANA, “maneno niliyoyatuma kwao mara kwa mara kupitia kwa watumishi wangu manabii. Wala ninyi watu wa uhamisho hamkusikiliza pia,” asema BWANA. Kwa hiyo, sikieni neno la BWANA, enyi nyote mlio uhamishoni, niliowapeleka Babeli kutoka Yerusalemu. Hili ndilo BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, asemalo kuhusu Ahabu mwana wa Kolaya, na Sedekia mwana wa Maaseya, wanaowatabiria uongo kwa jina langu: “Nitawatia mikononi mwa Nebukadneza mfalme wa Babeli, naye atawaua mbele ya macho yenu hasa. Kwa ajili yao, watu wote wa Yuda walio uhamishoni Babeli watatumia laana hii: ‘BWANA na akutendee kama Sedekia na Ahabu, ambao mfalme wa Babeli aliwachoma moto.’ Kwa kuwa wamefanya mambo maovu kabisa katika Israeli, wamezini na wake za majirani zao, tena kwa Jina langu wamesema uongo, mambo ambayo sikuwaambia kuyafanya. Nami nayajua haya, na ni shahidi wa jambo hilo,” asema BWANA.