Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Isaya 65:1-16

Isaya 65:1-16 NEN

“Nilijifunua kwa watu wale ambao hawakuniulizia. Nimeonekana na watu wale ambao hawakunitafuta. Kwa taifa lile ambalo halikuliita Jina langu, nilisema, ‘Niko hapa, niko hapa.’ Mchana kutwa nimeinyoosha mikono yangu kwa watu wakaidi, wanaokwenda katika njia ambazo si nzuri, wafuatao mawazo yao wenyewe: taifa ambalo daima hunikasirisha machoni pangu, wakitoa dhabihu katika bustani na kufukiza uvumba juu ya madhabahu za matofali; watu waketio katikati ya makaburi na kukesha mahali pa siri, walao nyama za nguruwe, nazo sufuria zao zina mchuzi wa nyama zilizo najisi, wasemao, ‘Kaa mbali; usinikaribie, kwa maana mimi ni mtakatifu mno kwako!’ Watu wa aina hiyo ni moshi katika pua zangu, ni moto uwakao mchana kutwa. “Tazama, jambo hili hubakia limeandikwa mbele zangu: sitanyamaza, bali nitalipiza kwa ukamilifu; nitalipiza mapajani mwao: dhambi zenu na dhambi za baba zenu,” asema BWANA. “Kwa sababu walitoa dhabihu za kuteketezwa juu ya milima na kunichokoza mimi juu ya vilima, nitawapimia mapajani mwao malipo makamilifu kwa matendo yao ya zamani.” Hili ndilo asemalo BWANA: “Kama vile divai mpya ingali bado inapatikana katika kishada cha zabibu, nao watu husema, ‘Usikiharibu, kwa kuwa bado kuna kitu kizuri ndani yake,’ hivyo ndivyo nitakavyofanya kwa ajili ya watumishi wangu; sitawaangamiza wote. Nitawaleta wazao kutoka kwa Yakobo, na kutoka kwa Yuda wale watakaomiliki milima yangu, nao watu wangu wateule watairithi, nako huko wataishi watumishi wangu. Sharoni itakuwa malisho kwa ajili ya makundi ya kondoo, na Bonde la Akori mahali pa kupumzikia kwa makundi ya ngʼombe, kwa ajili ya watu wangu wanaonitafuta. “Bali kwenu ninyi mnaomwacha BWANA na kuusahau mlima wangu mtakatifu, ninyi mnaoandaa meza kwa ajili ya Bahati, na kujaza mabakuli ya mvinyo uliochanganywa kwa ajili ya Ajali, nitawaagiza mfe kwa upanga, nanyi nyote mtainama chini ili kuchinjwa; kwa kuwa niliwaita lakini hamkuitika, nilisema lakini hamkusikiliza. Mlitenda maovu machoni pangu, nanyi mkachagua mambo yale yanayonichukiza.” Kwa hiyo hili ndilo asemalo BWANA Mwenyezi: “Watumishi wangu watakula, lakini ninyi mtaona njaa; watumishi wangu watakunywa lakini ninyi mtaona kiu; watumishi wangu watafurahi, lakini ninyi mtaona haya. Watumishi wangu wataimba kwa furaha ya mioyo yao, lakini ninyi mtalia kutokana na uchungu wa moyoni, na kupiga yowe kwa sababu ya uchungu wa roho zenu. Mtaliacha jina lenu kuwa laana kwa watu wangu waliochaguliwa; BWANA Mwenyezi atawaua ninyi, lakini watumishi wake atawapa jina jingine. Yeye aombaye baraka katika nchi atafanya hivyo kwa Mungu wa kweli; yeye aapaye katika nchi ataapa kwa Mungu wa kweli. Kwa kuwa taabu za zamani zitasahaulika na kufichwa kutoka machoni pangu.

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Isaya 65:1-16

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha