Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Isaya 15:1-9

Isaya 15:1-9 NENO

Neno la unabii kuhusu Moabu: Ari iliyo Moabu imeangamizwa: imeharibiwa kwa usiku mmoja! Kiri iliyo Moabu imeangamizwa, imeharibiwa kwa usiku mmoja! Diboni anakwea hadi kwenye hekalu lake, hadi mahali pake pa juu pa kuabudia ili walie, Moabu anaombolezea Nebo na Medeba. Kila kichwa kimenyolewa na kila ndevu limeondolewa. Wamevaa magunia barabarani; juu ya mapaa na kwenye viwanja wote wanaomboleza, wakilala kifudifudi na kulia. Heshboni na Eleale wanalia, sauti zao zinasikika hadi Yahazi. Kwa hiyo watu wenye silaha wa Moabu wanapiga kelele, nayo mioyo yao imezimia. Moyo wangu unamlilia Moabu; wakimbizi wake wanakimbilia Soari, hadi Eglath-Shelishiya. Wanapanda njia ya kwenda Luhithi, wanaenda huku wanalia; barabarani iendayo Horonaimu wanaombolezea maangamizi yao. Maji ya Nimrimu yamekauka na majani yamenyauka; mimea imekauka wala hakuna kitu chochote kibichi kilichobaki. Kwa hiyo mali waliyoipata na kujiwekea akiba wamezichukua na kuvuka Bonde la Mierebi. Mwangwi wa kilio chao umefika hadi mpakani mwa Moabu, kilio chao cha huzuni kimefika hadi Eglaimu, maombolezo yao hadi Beer-Elimu. Maji ya Dimoni yamejaa damu, lakini bado nitaleta pigo jingine juu ya Dimoni: simba juu ya wakimbizi wa Moabu na juu ya wale wanaobaki katika nchi.