Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Hosea 11:1-11

Hosea 11:1-11 NENO

“Israeli alipokuwa mtoto, nilimpenda; nilimwita mwanangu kutoka Misri. Lakini kadiri nilivyomwita Israeli, ndivyo walivyoenda mbali nami. Walitoa dhabihu kwa Mabaali na kufukiza uvumba kwa vinyago. Mimi ndiye niliyemfundisha Efraimu kutembea, nikiwashika mikono; lakini hawakutambua kuwa ni mimi niliyewaponya. Niliwaongoza kwa kamba za huruma ya kibinadamu, kwa vifungo vya upendo; niliondoa nira shingoni mwao nami nikainama kuwalisha. “Je, hawatarudi Misri, nayo Ashuru haitawatawala kwa sababu wamekataa kutubu? Upanga utavurumishwa katika miji yao, nao utaharibu makomeo ya malango yao na kukomesha mipango yao. Watu wangu wamedhamiria kuniacha. Hata wakimwita Yeye Aliye Juu Sana, kwa vyovyote hatawainua. “Efraimu, ninawezaje kukuacha? Ee Israeli, ninawezaje kukutoa? Nitawezaje kukutendea kama Adma? Nitawezaje kukufanya kama Seboimu? Moyo wangu umegeuka ndani yangu, huruma zangu zote zimeamshwa. Sitatimiza hasira yangu kali, wala sitageuka na kumharibu Efraimu. Kwa kuwa mimi ndimi Mungu, wala si mwanadamu, Aliye Mtakatifu miongoni mwenu. Sitakuja kwa ghadhabu. Watamfuata BWANA; atanguruma kama simba. Anaponguruma, watoto wake watakuja wakitetemeka kutoka magharibi. Watakuja wakitetemeka kama ndege wakitoka Misri, kama hua wakitoka Ashuru. Nitawafanya waishi katika nyumba zao,” asema BWANA.